Wednesday, 2 March 2016

KATIBU WA CCM MKOA WA IRINGA AZUNGUMZIA KASHFA YA VIWANJA VYA UVCCM IRINGA


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimeiagiza ofisi ya Mkurugenzi ya Manispaa ya Iringa kutojihusisha na utoaji hati za baadhi ya viwanja vya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa vinavyodaiwa kuuzwa kinyemela.

Kwa zaidi ya miezi mitatu sasa kumekuwepo na taarifa zinazokanushwa na baadhi ya viongozi wa UVCCM za uuzaji wa baadhi ya viwanja katika shamba la umoja huo lililopo Igumbilo, mjini Iringa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema katika shamba hilo kuna viwanja zaidi ya 145 ambavyo baadhi yake kuna minong'no kwamba vimeuzwa kinyemala pasipo kuzingatia utaratibu.

“Kama kweli kuna mtu amenunua kiwanja pale Igumbilo ajue ameliwa, hawezi kupata kiwanja hicho kwasababu kama aliuziwa ajue aliuziwa nje ya taratibu za UVCCM na chama,” alisema.

Mtenga alisema kabla ya uuzaji huo ilipaswa vikao husika viketi kikiwemo kikao cha Kamati ya utekelezaji ambacho naye ni mjumbe na kukubaliana sababu za kufanya hivyo kabla ya kuomba idhini taifani.

“Baada ya maamuzi ya vikao, UVCCM walipaswa kuomba kibari cha uuzaji viwanja hivyo kwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa wakieleza pia sababu ya kutaka kuuza baadhi ya viwanja hivyo na kusubiri idhini ya Taifa,” alisema.

Alisema hakuna mali ya chama hicho inaweza kuuzwa pasipo kuridhiwa na Baraza la Wadhamini wa chama kwahiyo kama kuna mtu aliuziwa kinyume na utaratibu huo amtafute aliyemuuzia ili amdai fedha zake.

Alisema kama kuna vijana waliuza viwanja hivyo kinyemela wanatakiwa kurudisha fedha za watu ili wasiingie kwenye matatizo makubwa lakini na wale waliouziwa wajitokeze ili waweze kukisaidia chama kujua ukweli wa suala hilo.

“Waliouziwa waje na nyaraka zinazoonesha kwamba waliuziwa viwanja hivyo na wanaohusika na uuzaji huo. Tunataka kujua nani alinunua, kwa gharama gani na nani aliyemuuzia ili kama kweli tukate mzizi wa fitina,” alisema.

Wakati huo huo, Mtenga alisema vikao vya maadili vya ngazi zote za chama hicho mkoani Iringa vinaendelea kuzifanyia kazi tuhuma mbalimbali zikiwezo za usaliti zinazowakabili baadhi ya wanaCCM wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu, mwaka jana.

Alisema kazi ya kuwahoji watuhumiwa wa usaliti inafanywa kwa ustadi mkubwa ili kusiwepo na malalamiko ya kuonewa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment