Thursday, 10 March 2016

KASESELA ATETEA HAKI ZA WAFANYAKAZI MAJUMBANI NA WAHUDUMU WA BAR


MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amesema muda wa kutetea haki ya malipo ya kila mwezi kwa wafanyakazi wa majumbani na bar umefika na unapaswa kufanywa kwa nguvu kubwa.

Ili kuondokana na udanganyifu wa waajiri wa makundi hayo ya watu kuna haja ya kuwepo kwa utaratibu utakaowalazimisha kufanya malipo ya wafanyakazi hao kupitia benki.

Akizungumza na wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Mahoteli, Majumbani, Huduma za Jamii na ushauri (Chodawu) mjini Iringa juzi, Kasesela alisema zipo taarifa za kutosha zinazohusu wafanyakazi hao kunyanyaswa na kuteswa.

Mbali na kunyanyaswa na kuteswa alisema wafanyakazi hao wamekuwa wakifanyia vitendo vinavyowadhalilisha na wananyimwa haki zao hali inayofanya maisha ya wengi wao yaendelee kuwa duni na wakati mwingine ya kificho.

Alisema mapambano dhidi ya umasikini hayawezi kufanikiwa kama makundi hayo na mengine yanayoapata vipato vidogo yataendelea kudhulumiwa haki zao.

Mwaka 2013, Chodawu kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani(ILO) Tanzania walizindua kampeni kupitia vyombo vya habari juu ya umuhimu wa kazi za staha kwa wafanyakazi hao.

Lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kulinda na kuhifadhi haki za msingi za wafanyakazi hao ikiwamo ya upatikanaji wa mikataba ya maandishi na likizo za uzazi sambamba na ugonjwa, kwani ni mambo ambayo wamekuwa wakinyimwa kwa kipindi kirefu.

Kasesela alisema, sekta ya wafanyakazi wa majumbani na bar muhimu katika ustawi wa familia, uchumi na nchi kwa jumla, lakini ni moja kati ya sekta inayokabiliwa na changamoto nyingi ingawa mbinu mbalimbali zimeshawahi kutumika kuona haki za makundi hayo zinapatikana.

“Kama wewe ni mwajiriwa iwe wa sekta binafsi au umma na una familia inayohitaji uangalizi wa karibu katika kipindi ambacho unakuwa kazini , basi kuajiri mfanyakazi wa nyumbani ni suala lisiloepukika katika maisha yako ya kila siku. Cha kushangaza wengi wetu, tunawafanyia mambo yasiyostaili”, alitofa mfano.


Katika kukabiliana na changamoto hizi Chodawu imeitaka Serikali kuharakisha uridhiaji wa mkataba wa kimataifa namba 189 pendekezo namba 201 unaozungumzia mambo muhimu ya wafanyakazi wa majumbani. 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment