Sunday, 6 March 2016

BALOZI WA NORWAY NCHINI AZINDUA SHULE YA AWALI ILULA, KILOLOBALOZI wa Norway nchini, Hanne-Marie Kaarstad juzi amezindua shule ya awali ya Sollerud ambayo imejengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 335 katika makao makuu ya Programu ya Watoto Yatima Ilula (IOP), katika kijiji cha masukanzi, wilayani Kilolo mkoani Iringa.

Shule hiyo imejengwa kwa msaada wa wasamaria wema wa nchini Norway ikiwemo shule dada ya Sollerud na mashirika ya YMCA na YWCA kwa lengo la kutoa elimu bora kwa watoto na kutoa stadi za maisha na uchumi kwa wasichana waliokatiza masomo baada ya kupata mimba.

Wakilenga kusaidia kukabili tatizo la usafiri kwa wanafunzi wa shule hiyo, wadau mbalimbali walioshiriki uzinduzi wake, akiwemo balozi huyo, mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesera na Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto walitoa ahadi ya mchango wa zaidi ya Sh Milioni 22 utakaoisaidia shule hiyo kununua basi la kubeba wanafunzi hao ambalo thamani yake ni zaidi ya Sh Milioni 50.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika liliso la kiserikali la Mpango wa Kusaidia watoto Yatima Ilula (IOP) linaloendesha shule hiyo na kituo hicho, Edson Msigwa, alisema shule hiyo yenye uwezo wa kuchukua watoto 120 n wasichana wanaopata mimba katika umri mdogo 40 ina vyumba vinne vya madarasa, ofisi, maktaba na ukumbi mmoja.

Akizindua shule hiyo yenye kituo cha kuwaendeleza wasichana waliopata mimba wakiwa na umri mdogo juzi, balozi huyo alisema serikali ya Norway inaridhishwa na juhudi za serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya elimu na kuahidi kusaidia kutatua changamoto zilizopo.

Akimpongeza Rais Dk John Magufuli kwa kutekeleza mpango wa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, alisema shule hiyo itawafungulia fursa za kimaisha watoto na wasichana hao, sio kwa kujifunza na kuandika pekee, bali kuwawezesha kuwa na misingi itakayojenga maisha yao ya baadaye, kujiheshimu, kupambana na changamoto zinazowazunguka na kuuungana katika masuala mbalimbali yanayohusu jamii yao.

“Ili watoto wakue katika maadili mema, wanatakiwa kufundishwa kushirikiana na wenzao katika mambo mema, kucheza pamoja, kutowachukia wengine, kutokuwa wadokozi, kuomba msamaha, kuosha mikono kabla ya kula na mengine mengi,” alisema.

Alisema watu zaidi ya Bilioni 1.2 duniani kote wanaishi maisha ya umasikini kwasababu walikosa msingi wa elimu ya kujikomboa.

Balozi Kaarstad alisema ili Tanzania iweze kupambana vilivyo na umasikini wa watu wake na Taifa kwa ujumla ni lazima iwekeze kwa watoto kwa kuendelea kuboresha mfumo wake wa elimu.

Alisema Norway ambayo katika maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini imejikita zaidi kuchangia elimu ya ufundi stadi, katika bunge lake la mwaka 2014 ililridhia kuongeza kwa asilimia 100 misaada yake katika sekta ya elimu duniani.


Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza , Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela ameishukuru serikali ya Norway na wadau wake kwa kujenga shule hiyo na kusema itatoa ushirikiano kwa kujenga barabara ya kuelekea shuleni hapo na kuhakikisha tatizo la maji linatafutiwa ufumbuzi hoja iliyoungwa mkono na mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment