Wednesday, 2 March 2016

BAADHI YA WAFANYABIASHARA IRINGA WAHAHA BAADA YA TFDA KUNASA MANUKATO FEKISIKU moja baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kubaini uwepo wa kiwanda cha kuzalisha vipodozi na manukato bandia, Kigamboni Jijini Dar es Salaam, wafanyabishara wa bidhaa hizo mjini hapa wameanza kuziondoa katika maduka yao, bidhaa zinazofanana na hizo.

Mtandao huu, ulitembelea baadhi ya maduka ya vipodozi mjini hapa na kushuhudia baadhi yao wakizifunga bidhaa hizo kwenye maboksi kama vile zimenunuliwa na wateja wao.

Mmoja wa wafanyakazi katika moja ya maduka hayo aliuambia mtandao huu kwamba; “bosi anajihami baada ya kusikia taarifa ya manukato feki kukamatwa jijini Dar es Salaam.”

Kwahiyo jana usiku na leo asubuhi tulikuwa tunafanya zoezi la kurudishia baadhi ya bidhaa hizo kwenye maboksi na sijui zitapelekwa wapi, alisema kijana huyo kwa sharti la kutotaja jina lake.

Katika tukio la jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hill Sillo alisema mamlaka hiyo imefanikiwa kubaini uwepo wa kiwanda hicho baada ya kupewa taarifa na wasamaria wema.

Sillo ameongeza kuwa taarifa hizo ziliwasaidia pia kukamata moja kati ya maduka katika maeneo ya  Sinza Kijiweni yanayouza manukato feki kutoka katika kiwanda hicho kinachomilikiwa na Dk. Mohammed Gwao.

“Tulifanikiwa kukamata jumla ya chupa 5350 za manukato bandia yenye thamani ya Shilingi milioni 107 yakiwa yamezalishwa katika kiwanda hicho na kuwekewa nembo inayoonesha kuwa yamezalishwa nje ya nchi,” aliongeza.

Katika mahojiano na Dk Gwao juu ya vipodozi bandia vilivyokutwa ndani ya duka lake, alidai kuwa bidhaa hizo ameziagiza kutoka nchini Uturuki kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).

“Hata hivyo TFDA ilimtaka atoe vielelezo vya kuthibitisha uingizaji wa bidhaa hizo lakini alishindwa kufanya hivyo,” aliongeza Sillo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment