Wednesday, 23 March 2016

ACT WAZALENDO YATAKA SPIKA ASHUGHULIKIE SUALA LA WABUNGE WANAOTUHUMIWA KWA RUSHWA


CHAMA cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko uamuzi uliofanywa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kwa kuhamisha kamati, Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Wajumbe wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge uliofanywa jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa ACT Wazalendo, Yeremia Maganja, amesema uamuzi huu wa spika unafuatia kashfa nzito ya viongozi na wajumbe wa kamati mbalimbali za Bunge kupokea rushwa kutoka mashirika tofauti ya umma kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari

Amesema bunge ni mhimili wenye jukumu la kuisimamia serikali , hivyo baadhi ya wabunge akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) walimwandikia barua za kujiuzulu Spika wa Bunge, Job Ndugai ili kupisha uchunguzi ufanyike na wataobainika kupokea rushwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Maganja amesema ACT Wazalendo imempongeza Mbunge wao na Wabunge wengine waliochukua hatua ya kujiuzulu ujumbe kwenye kamati zao ili kupisha uchunguzi.

Aidha amesema kuwa uamuzi huo wa mbunge wao unakwenda sambamba na misingi ya Chama cha ACT Wazalendo ya uadilifu na uwajibikaji.

Amesema mabunge yaliyopita, kamati za Bunge zimekuwa zikituhumiwa mara kadhaa kujihusha na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa Mashirika ya Umma, Makampuni na watu binafsi.

Maganja amesema rai zimekuwa zikitolewa mara kwa mara huko nyuma ya kuitishwa kwa uchunguzi ili kulinda hadhi na heshima ya Bunge ilipuuzwa na matokeo yake, kashfa hizi zimeliondolea heshima Bunge na Wabunge.

Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge ndiyo chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake. 


Kinapotuhumiwa kupokea rushwa, kinawezaje chenyewe kuisimamia serikali na kuongoza mapambano dhidi ya rushwa?

Maganja amesema uamuzi wa kuwahamisha Kamati viongozi na wajumbe wa Kamati zilizotuhumiwa kupokea rushwa ni sawa na kuufunika uozo na kuendeleza utamaduni mbovu wa siku nyingi hapa nchini wa kuwahamisha au “kuwapangia kazi nyingine” viongozi na watumishi wa umma wanaotuhumiwa kupokea rushwa au kukosa ufanisi. 


Kimsingi Utamaduni huu unafifisha mapambano dhidi ya rushwa na uwajibikaji.

Mwenyekiti huyo amemtaka Spika kuonyesha kwa vitendo jinsi ofisi yake inavyochukizwa na vitendo vya rushwa nchini kwa kuitisha uchunguzi utaovishirikisha vyombo vya dola ili ukweli ujulikane.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment