Saturday, 27 February 2016

ZITTO ATAKA MALI NA MADENI YA VIONGOZI ZIWE TAARIFA ZA WAZI


Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amemtaka Rais Dkt. John Magufuli kuiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuweka mtandaoni fomu za mali na madeni ya viongozi wa umma ili kila mtu aweze kuziona.

Zitto ametoa kauli hiyo siku moja baada ya baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kusukumwa na Rais Magufuli kuwasilisha Tamko la Rasilimali, Maslahi, Madeni pamoja na Uadilifu kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kufanikiwa kufanya hivyo dakika za mwisho baada ya kuwekewa muda maalum wa kikomo.

Amesema Rais Magufuli aagize mali na madeni ya viongozi wa umma yawekwe wazi kwenye tovuti ya Tume ya Maadili ya Viongozi.

“Sheria irekebishwe watu wanaotoa matamko kuweka wazi, bila uwazi ni vigumu kupambana na rushwa,” aliandika mwanasiasa huyo katika ukurasa wake wa Facebook.


Zitto Kabwe ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, amekuwa akisisitiza kuwa msimamo wa chama chake ni kuhakikisha maadili yanazingatiwa na vionggozi na katiba ya chama inamtaka kila kiongozi kutangaza mali na madeni yake kwa uwazi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment