Thursday, 11 February 2016

WASIRRA AZUNGUMZIA UKUBWA WA SERIKALI YA MAGUFULI

Stephen Wasira

Waziri wa Zamani wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira amezodoa muundo wa wizara za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli akisema hana uhakika kama unabana matumizi kama inavyoelezwa ikilinganishwa na serikali zilizopita.

Amesema kuna baadhi ya wizara zimepewa jina moja lakini kimantiki kuna wizara mbili ndani yake na hii inaonyesha kuwa hakuna matumizi yoyote yaliyopungua bali ni kubadili jina la wizara tu.

Akitolea mfano Wizara ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa, Utumishi na Utawala Bora, amesema ni wizara moja lakini yenye mawaziri wawili.

Waziri mmoja anasimamia utumishi na utawala bora na mwingine anasimamia tawala za mikoa na serikali za mitaa, sasa hiyo wizara ni moja?, alihoji Wasira ambaye alichukua fomu za kuwania nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka jana katika mahojiano maalum na gazeti la Mwananchi.

“Kila wizara ina katibu mkuu wake, kwa hiyo ni wizara mbili zimepewa jina moja na kwa hivyo nikijumlisha naona wizara 19 na mawaziri 19,” aliongeza.

Wasira aliongeza kuwa ingawa hana uwezo wa kupiga mahesabu na kuthibitisha kutumia wizara zote endapo muundo huo wa baraza la mawaziri umebana matumizi ama la, anaweza kutumia wizara mbili ili kutoa picha ya jambo hilo.

“Hapa sina kikokotozi, lakini naweza kutoa maoni kwenye wizara mbili, moja ya kilimo ninayoijua zaidi, ambayo imeunganishwa na mifugo na uvuvi na ambayo ina makatibu wakuu watatu,” alifafanua.

Mifugo ina katibu mkuu wake, kilimo ina katibu mkuu wake na uvuvi ina katibu mkuu wake, sasa hivi kweli unahitaji calculator ili kujua kama gharama za kuendesha Serikali zimepungua au kuongezeka kwasababu huko nyuma kulikuwa na mawaziri wawili na makatibu wakuu wawili basi.

Wasira amekuwa waziri wa tatu katika Serikali iliyopita kujitokeza hadharani na kukosoa muundo wa baraza la mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano kwa ulinganifu na ubanaji matumizi, baada ya Bernard Membe na Dr. Makongoro Mahanga.

Katika hatua nyingine, Wasira amemshauri Rais Magufuli kuitoa idara ya umwagiliaji kutoka Wizara ya Maji na kuirudisha Wizara ya Kilimo ilipokuwa mwanzo kwasababu umwagiliaji ni sehemu ya kilimo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment