Friday, 19 February 2016

WAKANDARASI WA IRINGA NA NJOMBE KUUNGANISHA KAMPUNI ZAO
WAKANDARASI zaidi ya 50 wa mikoa ya Iringa na Njombe wako katika hatua ya kuunganisha nguvu zao ili wawe na kampuni chache hatua itakayowawezesha kuongeza ufanisi tofauti na ilivyosasa kwa kila mmoja kufanya kazi kivyake.

Katika kikao chao kilichofanyika mjini Iringa hivikaribuni, wakandarasi hao walisema endapo utafanikiwa, uamuzi huo utawawezesha pia kukabiliana na bugudha ya kuombwaombwa rushwa na baadhi ya wasimamizi wa miradi hasa ya serikali.

“Baadhi ya wakandarasi, sio wote, wanatoa sana rushwa ili wapate kazi, na baadhi ya watendaji wa serikali wamegeuza rushwa kama mradi wao halali kabla na baada ya wakandarasi hao kupata kazi,” alisema mmoja wao kwa sharti la kutotaja jina.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakandarasi Mkoa wa Iringa, Vitus Mushi alisema kama tuhuma za kuombwa rushwa ni za kweli, dawa pekee kwa wakandarasi hao ni kukubaliana na pendekezo la kuungana.

“Faida za kuungana ni nyingi sana, kutatuwezesha kubadilishana uzoefu, kukuza mtaji, kuongeza vifaa na kuajiri wataalamu hatua itakayotusaidia kuwa na vigezo mbalimbali muhimu vinavyotakiwa kwa kampuni za ukandarasi,” alisema.

Mushi alisema sio siri kwamba kampuni nyingi za ukandarasi zinapata kazi kwa kubebwa na watendaji kwasababu kiuhalisia hazikidhi baadhi ya vigezo muhimu vinavyotakiwa iliwapate kazi hizo.

“Kwahiyo hata haya ya rushwa yanayolalamikiwa kuhusu watendaji hao huenda yakawa ya kweli kwasababu yanafanywa kwa pamoja na wakandarasi kwa msingi wa kubebana pande zote mbili,” alisema.

Alisema katika baadhi ya maeneo nchini ambayo wakandarasi wamekubali kuunganisha nguvu zao, inashuhudiwa jinsi wanavyopata kazi kubwa kwa kuwa vigezo wanavyo na zinaendelea kuwawezesha kuboresha kampuni zao na maisha yao wenyewe.

Akizungumzia uzoefu, mmoja wa wakandarasi hao, Edwin Sambala alisema; “maisha ya wakandarasi wengi wa mkoa wa Iringa na Njombe hayabadiliki kwasababu kazi nyingi tunazopata hazilipi kwakuwa zinafanywa kwa malipo madogo ili mradi tu tuonekane tunafanya kazi.”

Kwa pamoja wakandarasi hao, walikubaliana na wazo la kuungana huku wakisema wataunganisha kampuni kati ya moja na 10 kulingana na uwezo wao na jinsi wanavyoaminia.

Pamoja na kuungana, Meneja wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Wakandarasi hao, Julius Masue aliwataka wale ambao si wanachama wake kujiunga na asasi hiyo ya kifedha kwakuwa ina masharti nafuu ya mikopo tofauti na taasisi zingine za kifedha kama mabenki.

Katika hatua nyingine, wakandarasi hao wamesema hawaoni kama ni sahihi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufunga ofisi za baadhi ya wakandarasi wanaochelewa kulipa kodi mbalimbali za serikali kwasababu kosa hilo mara kwa mara limekuwa likisababishwa na serikali yenyewe pale inapochelewa kuwalipa madeni yao yatokanayo na kazi walizofanya.

“Sasa kama serikali inachelewesha malipo kwa wakandarasi kwanini serikali hiyo hiyo ituchukulie hatua pale tunaposhindwa kulipa kodi zake kwa wakati,” aliuliza Katibu wa wakandarasi hao, Mathias Magigita.

Magigita alisema wapo wakandarasi wanaoidai serikali zaidi ya Sh Milioni 100, huku wao wakidaiwa na TRA chini ya Sh Milioni 10 lakini wamekuwa wakiadhibiwa kwasababu ya hekima kushindwa kutumika.

Wakati huo huo, wakandarasi hao wameahidi kutoa taarifa za siri serikalini zinazowahusu baadhi ya wahandisi na watendaji katika halmashauri na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wenye kampuni za siri zinazopta kazi katika maeneo yao ya kazi.


Wakati baadhi ya kampuni za watendaji hao zikipata kazi kabla hata hazijamiliza kazi za awali, wakandarasi hao walisema kampuni zingine zinasota zaidi ya miaka miwili bila kupata kazi pamoja na kutumia fedha nyingi kununua na kuandaa vitabu vya tenda.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment