Wednesday, 10 February 2016

WAGONJWA WA KIPINDUPINDU WAONGEZEKA IRINGA, MMOJA AFARIKI


IDADI ya watu waliokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika kijiji cha Mboliboli wilayani Iringa imengozeka kutoka 20 hadi 85 jana asubuhi, huku moja kati yao akiripotiwa kufa.

Wagonjwa 18 kati ya wagonjwa hao wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu na wengine wanaendelea na matibabu hayo katika Zahanati ya St Lukes kijijini hapo.

Ili kuudhibiti ugonjwa huo Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ametoa maagizo mbalimbali likiwemo lile linalowataka wananchi kuacha kula kachumbari, matunda yasiooshwa, viporo na vyakula vilivyopoa.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Masenza alisema taarifa zinaonesha ugonjwa huo umewakumba vibarua waliokwenda kulima mashamba ya mpunga katika eneo hilo huku wakiwa na mazoea ya kunywa bila kuchemsha maji ya mfereji wa umwagiliaji ambayo si salama.

“Katika mashamba hayo hakuna vyoo, hivyo hali ya usafi wa mazingira siyo nzuri na vyanzo vingi vya maji vimechafuliwa,” alisema na kuongeza kwamba wengi wa vibarua hao wanatoka wilayani Kilolo, mkoani Iringa.

Alitoa wito kwa wananchi wakiwemo wa manispaa ya Iringa kuacha kutumia maji ya madimbwi, mito na mifereji na badala yake watumie maji kutoka vyanzo salama kama visima na mabomba.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe alisema katika kujihadhari na ugonjwa huo manispaa yake inawataka wafanyabiashara wa vyakula barabarani kusimamisha biashara hizo kwasasa.

Kuhusu vilabu vya pombe za kienyeji, Kimbe alisema vinatakiwa kufungwa kwasababu vina hali mbaya na vinaweza kuwa chanzo cha mlipuko wa ugonjwa huo.

“Tunaomba wananchi wa Iringa watusamehe, biashara zinazotakiwa kufungwa zitarudi baada ya kupata taarifa za wataalamu kama kuwepo kwake hazitasababisha mlipuko huo, vinginevyo zitadhibitiwa kwa nguvu kama hiari inayotokana natangazo rasmi la serikali haitatekelezwa,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa alitoa pole kwa wananchi wa Mboliboli na familia za watu waliokumbwa na ugonjwa huo huku akiwataka watekeleze maagizo yote ambayo serikali imetoa kupitia viongozi wake ili kujinusuru na janga hilo.

“Tukizembea mkoa mzima wa Iringa utalipuka. Tushirikiane katika kupambana na janga hili ili lisienee,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment