Tuesday, 9 February 2016

VINYESI MASHAMBANI VYALETA KIPUNDUPINDU WILAYANI IRINGA


WAKAZI wa kijiji cha Mbolimboli, tarafa Pawaga wilayani Iringa mkoani Iringa wamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo hadi jana watu 20 waliripotiwa kuwekwa karantini kijijini hapo, wakiugua ugonjwa huo.

Akizungumza na HabariLeo jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Robert Salim alisema ugonjwa huo umelipuka baada ya eneo hilo kukumbwa na mafuriko.

“Mafuriko hayo yamesababisha uchafu wa vyoo vilivyobomoka, watu kujisaidia mashambani na vichakani na uchafu huo kusambaa hadi kwenye maji yanayotumiwa na wakazi wa eneo hilo,” alisema.

Alisema wagonjwa hao 20 wamepokelewa na kuweka katika kambi maalumu kijijini hapo wakiwa wanatapika na kuharisha mfululizo.

Alisema waliothiriwa na ugonjwa wengi wao ni wakazi wa wilaya ya Kilolo waliokuwa wamekwenda katika kijiji hicho kufanya kazi ya vibarua katika mashamba ya mpunga.

Alisema wizara ya afya imewasaidia kwa kuwapatia dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kunusuru maisha ya watu hao.

Dk Salim alisema kama wananchi wasiposhiriki kuudhibiti ugonjwa huo upo uwezekano wa kusambaa katika maeneo mengi ya mkoa wa Iringa.

“Halmashauri zote zimekwishajulishwa kuchukua tahadhari na kuelimisha jamii kuzingatia usafi, matumizi ya vyoo bora na kutokula ovyo ovyo ili kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema.

Alisema halmashauri hizo zinatakiwa kufunga sehemu za biashara za vyakala zinazoendeshwa katika mazingira ya uchafu na wahudumu ambao hawajapima afya zao.


“Agizo hilo linatakiwa kwenda sambamba na kuudhibiti uuzaji wa vyakula na matunda yaliyomenywa katika sehemu zisizoruhusiwa,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment