Wednesday, 10 February 2016

SERIKALI YAZIKOMALIA BARABARA ZA MZUNGUKO JIJINI DAR ES SALAAM

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akifafanua hatua za Serikali za kuhakikisha ujenzi wa barabara za mzunguko Jijini Dar es Salaam unakamilika mwezi juni mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa barabara za mzunguko (ring roads) zenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam utakamilika Mwezi Juni, mwaka huu.

Amesema hilo litawezekana baada ya Serikali kuanza kulipa madeni ya makandarasi na kuwataka  wote kurudi kazini ili kufikia lengo la Serikali la kukamilisha barabara hizo mwezi Juni sambamba na ulipaji wa madeni yote.

“Tunawaomba wale wote wenye nyumba pembezoni mwa barabara za mzunguko na ambao wapo kwenye orodha ya kulipwa fidia waondoke maeneo hayo ili kuruhusu kazi ya ujenzi wa barabara kuendelea,” ameongeza Waziri Mbarawa.

Barabara za mzunguko Jijini Dar es Salaam zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kuvutia magari mengi kutumia barabara hizo na kupunguza msongamano katikati ya Jiji ambapo hadi sasa Kilomita 27 zimekamilika na Kilomita 28 zinaendelea kujengwa.

Waziri Prof. Mbarawa pia amekagua ujenzi wa daraja la Kinyerezi lenye urefu wa mita 40 lililojengwa kwa gharama ya sh. Bilioni 2.3 ambao ujenzi wake umekamilika.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale amewataka madereva kulinda barabara hizo kwa kutoegesha magari katika maeneo yasiyoruhusiwa na kukemea vitendo vya uchimbaji mchanga pembeni mwa madaraja.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment