Thursday, 4 February 2016

RC MASENZA NA JAJI SHANGALI WAWAPASHA MAWAKILI WA KUJITEGEMEA IRINGA


MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewaomba mawakili wa kujitegemea kuacha kuwatetea watu wanaofikishwa mahakamani kwa makosa yanayohusiana na ukwepaji wa kodi na matumizi mabaya ya fedha za umma ili kuonesha uzalendo kwa Taifa lao.

Kwa kupitia hotuba yake aliyoitoa jana kwenye maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Masenza alisema:

“Serikali itaendelea kukosa mapato yake stahiki kama wakwepa kodi na watumishi wasio waaminifu wanaotumia vibaya au kuipotezea serikali mapato yake wataendelea kutetewa mahakamani ili washinde kesi zao.

Huku mawakili waliokuwepo katika maadhimisho hayo wakicheka, mkuu wa mkoa huyo alisema serikali inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli zake za maendeleo kwasababu ya upungufu wa fedha ambazo sehemu yake zinapotea katika mikono ya walipa na watu wengine wasio waaminifu.

Mbali na kuboresha miundombinu ya mahakama kwa kiwango kinachotakiwa, Masenza alisema serikali inawajibu wa kukusanya mapato yake na kuyasimamia ipasavyo bila woga ili iweze kutoa huduma muhimu kwa wananchi wake zikiwemo za ujenzi wa nyumba za mahakimu na watoa huduma wengine wa idara mbalimbali za serikali.

Mbali na ombi hilo la mkuu wa mkoa naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mary Shangali aliwaomba mawakili hao wawape wananchi fursa ya kupata haki iliyo bora kwa kupunguza ada na gharama wanazotoza.

“Kama kweli wanataka huduma za haki zimlenge mwananchi, basi wajibu wao wa kwanza ni kupunguza ada na gharama zinazotozwa na wakati mwingine wawe tayari kuwasaidia bure wale wasio na uwezo,” alisema.

Jaji Shangali alisema mawakili wa kujitegemea ni wadau muhimu katika dhana ya huduma za haki kwa wananchi kwani wao ndio wanaowawakilisha na kuwasimamia mashauri yao mahakamani.

Alisema katika kanda ya Iringa kuna mawakili wa kujitegemea zaidi ya 45 na kati yao wapo ambao wanasahau kutekeleza majukumu yao ya uwakili mahakamani ipasavyo.

“Wapo mawakili ambao hawajiandai ipasavyo katika kuendesha mashauri ya wateja wao, hawatayarishi kesi za rejea na wengine hawajui historia ya kesi za wateja wao,” alisema.

Akitoa wito kwa mawakili hao kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi yao, Jaji Shangali alisema hali hiyo inasikitisha kwasababu wananchi hawataweza kupata huduma ya haki kama wanavyokusudia.


Maadhimisho haya ya sheria yanafanyika kwa mara ya 21 nchini kote tangu yaanzishwe mwaka 1996 yakiwa na madhumuni ya kuzindua shughuli za kimahakama kwa kipindi cha mwaka mpya, kuwaweka watumishi wa mahakama mikononi mwa Mungu kwa kuwaombea ili wafanye kazi zao kwa kuzingatia viapo na maadili yao ya kazi na kujifunza na kutoa elimu ya sheria kwa umma.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment