Monday, 22 February 2016

PPF YASAIDIA WAATHIRIKA WA MAFURIKO IRINGA, WAZIRI MKUU AWAPONGEZA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameupongeza Mfuko wa Pensheni wa PPF kwa msaada wake wa bati 200 na mifuko 200 ya saruji waliyotoa jana kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko wa Pawaga na Mboliboli, Iringa Vijijini.

Pamoja na PPF, waziri mkuu aliwapongeza wadau wengine wote waliojitokeza kusaidia waathirika hao na akawaalika wengine popote walipo kujitokeza kuchangia mahitaji makubwa ya watu hao.

“Serikali inawakaribisha popote mlipo, mjitokeze kuchangia watu waliokumbwa na mafuriko kwasababu mahitaji yao ni makubwa na wanahitaji msaada wa kila anayeguswa,” Waziri Mkuu alisema wakati akipokea taarifa fupi ya PPF katika moja ya banda lililojengwa kwa ajili ya makazi ya muda ya waathirika hao.

Akitoa taarifa ya msaada huo, Meneja Mahusiano wa PPF, Lulu Mengele alisema; “PPF tuna sera ya kusaidia katika jamii ikiwemo ile inayokumbwa na majanga mbalimbali.”

Mengele alisema msaada huo wa bati 200 na mifuko 200 ya saruji una thamani ya Sh Milioni 6.6.

Alisema pamoja na kuandikisha wanachama toka sehemu mbalimbali, ni wajibu wa PPF kuhakikisha jamii inayowazunguka inaishi katika mazingira mazuri.

“PPF tuna mfumo wa kuwahudumia watu waliojiajiri wenyewe na wale walio katika sekta rasmi kwa kuwawekea hifadhi inayoweza kuwasaidia pindi majanga yanapotokea,” alisema.

Alisema pamoja na kusaidia waathirika wa kata ya Pawaga na Idodi, PPF itatoa msaada wake kwa wahanga wa mafuriko katika maeneo mengine nchini.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera hivikaribuni inaonesha jumla ya kaya 145 zilizoathiriwa na mafuriko hayo kwa makazi yao kuharibiwa zinahitaji msaada ili kurudi katika maisha yao ya kawaida.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment