Thursday, 4 February 2016

NANE WASIMAMISHWA KAZI HOSPITALI YA WILAYA YA MUFINDI BAADA YA KIFO CHA MJAMZITO


WATUMISHI nane wa hospitali ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa akiwemo
Mganga Mkuu, Dk Nelson Mtajwa wamesimamishwa kazi kwa muda ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya kusababisha kifo
cha mama mjamzito na mtoto wake aliyefariki kabla hajifungua hospitalini hapo, mjini Mafinga.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Shaib Nnunduma amekiri kusimamishwa kazi kwa watumishi hao na kwamba hatma yao itategemea matokeo ya uchunguzi huo.
 
Mbali na Dk Mtajwa wengine waliosimamishwa kazi kwa mujibu wa mkurugenzi huyo ni pamoja na Prosper Kalinga , Greysoni Sanga, Ajue Kilingatu, Jackilini Mtavangu, Miraji Ngule, Sixter Nyenza, pamoja na dobi wa hospitali hiyo Nelsoni Nyenza.

Kusimamishwa kazi kwa watumishi hao kumekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kuunda timu ya uchunguzi iliyoyopewa jukumu la kufuatilia malalamiko ya wagonjwa dhidi ya baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo wanaotuhumiwa kufanya kazi kwa mazoea huku wakitumia lugha zisizofaa kwa wagonjwa.


Nnunduma alisema tayari watumishi hao wameandikiwa barua za kujielezea kuhusiana na tuhuma zinazowakabili ikiwemo ya kusababisha kifo cha mjamzito huyo.

Taarifa zinazoendelea kufanyiwa uchunguzi kutoka katika chanzo ambacho hakikutaka kutaja jina lake gazetini zimedai kwamba mmoja wa madobi wa hospitali hiyo (jina linahifadhiwa) amekuwa akitumiwa kufanya kazi za kitabibu kwa kile kilichoelezwa uwepo wake hospitalini hapo kwa muda mrefu umemfanya atumiwe kwa kufanya kazi zinazotakiwa kufanywa na wataalamu.

Chanzo hicho kilisema dobi huyo ambaye kazi yake kuu ni ufuaji wa mashuka na nguo zingine za hospitalini hapo alimfanyia upasuaji baada ya kufariki, Sauda Myinga aliyekwenda hospitalini hapo kujifungua.

Mama huyo (Sauda) alipokelewa hospitalini hapo hivikaribuni akitokea katika kituo cha kutolea huduma cha Nyololo, wilayani humo.


Taarifa hiyo inasema uzembe wa watoa huduma wenye ujuzi uliopelekea Sauda achelewe kufanyiwa upasuaji ulisababisha apoteze maisha yeye pamoja na mtoto wake.

Baada ya kufariki mjamzito huyo, baadhi ya watoa huduma wa hospitali hiyo wanatuhumiwa kumpa kazi ya kumfanyia upasuaji mama huyo ili kukitoa kiumbe ambacho pia kilifariki.

Akizungumza na wanahabari mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye naye akutaka kutaja jina kwa kuwa si msemaji wa familia alisema ndugu yao
alihamishiwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi mjini Mafinga baada ya kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida katika kituo cha huduma cha Nyololo.


“Tulilazimika kumsafirisha hadi hapa Mafinga ili aweze kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya wilaya, lakini matokeo yake ndiyo hayo,” alisema ndugu huyo.
 
Alisema baada ya kufika hospitalini hapo ndugu yao huyo alikaa siku tano bila ya kupata huduma ya upasuaji kama ilivyotarajiwa huku wauguzi wakimpa matumaini kwamba angeweza kujifungua kwa njia ya kawaida kwa kuwa alionesha dalili hizo ambazo hata hivyo hazikutajwa.

 
“Marehemu alikuwa akilalamika kusikia maumivu makali na kuomba afanyiwe upasuaji bila mafanikio na baada ya kuchunguzwa na madaktari iligundulika kwamba mtoto aliyeko tumboni amefariki,” alisema.Pamoja na taarifa ya mtoto wake kufariki akiwa tumboni, Sauda hakufanyiwa upasuaji kwa madai kwamba kiumbe hicho kingetoka chenyewe baada ya muda.

Huku machozi yakimtoka alisema ndugu yao aliachwaa na kiumbe hicho kwa siku nzima huku uchafu na harufu kali zikimtoka sehemu zake za siri hali iliyosababisha siku iliyofuta (Januari 11) naye aage dunia.

Baada ya ndugu yetu kuaga dunia, alisema walipewa mfua mashuka ili afanye upasuaji huo wa kumtengenisha mama na mtoto kwa kiasi cha Sh 40,000.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment