MWANAFUNZI wa sekondari ya Mlowa wilayani
Iringa, Eva Tolage (16) ambaye mwaka jana alimuandika barua Rais wa Marekani
Barack Obama akielezea kero zinazowakabili hasa watoto wa kike katika kijiji
chake na kujibiwa, ameiomba jamii kuungana naye katika kampeni ya Simama na Eva
iliyozinduliwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera kuwahamasisha
vijana kupaza sauti zao.
Kwa kupitia kampeni hiyo inayoratibiwa na
asasi ya kimataifa ya Restless Development kwa kushirikiana na kampeni ya kimataifa
ya kupambana na umasikini ya ONE Campaign, Eva anayesoma kidato cha pili katika
shule hiyo anawahimiza viongozi wa serikali na washirika wake wa maendeleo
kutekeleza ahadi mbalimbali za maendeleo wanazozitoa kwa wananchi.
Katika barua yake hiyo aliyoindika baada
ya kumaliza elimu ya msingi akiwa na miaka 15 wakati utekelezaji wa Mpango wa
Malengo ya Millenia (MDGS) ukimalizika na rais huyo akaijibu katika mkutano wa 70
wa Baraza la Umoja wa Mataifa wa Septemba mwaka jana uliojadili Maendeleo Endelevu
ya Dunia, Eva alisema:
“Mwaka 2015 ni mwaka unaotarajia kuweka
malengo endelevu ya maendeleo na ninataka kuuliza kama unaweza kufanya kitu
chochote kwa ajili ya maendeleo yangu binafsi na wasichana kwa ujumla duniani
kote.
Kwa kupitia barua hiyo ambayo juzi Eva
alirudia kuisoma mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa na viongozi wengine wa kata
na kijiji cha Mlowa katika tukio lililoandaliwa na Restless Development kijijini
hapo; Eva anayetaka kutimiza ndoto yake ya kuwa na elimu ya chuo kikuu amezungumzia
changamoto mbalimbali zinazomkwamisha yeye na wanafunzi wenzake kufikia malengo
yao.
Katika tukio hilo, Eva ambaye mwaka 2030 atakuwa
akitimiza miaka 30 muda ambao pia mpango wa Maendeleo Endelevu ya Dunia utakuwa
unamalizika alirudia kuzitaja changamoto zinazoikabili familia yake na kijiji
chake kwa ujumla kuwa ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama unaowaathiri
sana kimasomo kwani muda wanaotakiwa kuutumia kujisomea, hutumia kutembea
umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
Nyingine ni uhaba wa chakula kutokana na
athari za mabadiliko ya tabia nchi, nishati ya umeme vijijini ambayo bado haijawanufaisha
walengwa wengi na baadhi ya wasichana wenzake kukakatiza masomo wakiwa na umri
mdogo baada ya kuolewa huku wakikumbana na changamoto nyingine ya kutothaminiwa
na mawazo yao kutosikilizwa.
“Ningependa kuuliza wewe na viongozi
wengine wa dunia mtafanya nini kuhakikisha kila msichana katika kijiji changu na
Afrika anapata maji safi na salama, nishati ya umeme na kuhakikisha kuwa
malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia yanatimia?” aliuliza Eva katika barua yake
aliyomuandikia Rais Obama.
Akijibu barua ya Eva wakati akihutubia mkutano
huo wa mwaka jana, Rais Obama alisema viongozi wadunia wamekusikia wewe (Eva) na
mamilioni ya watu wengine duniani wenye mahitaji kama yako.
“Leo naongea na Eva na mamilioni ya watu
wengine wanaoishi kwenye mazingira kama ya Eva, tunawaona, tunawasikia, nimesoma
barua yako, na leo tunaweka dhamira ya kutekeleza mahitaji yenu kwa haraka kama
mataifa na kama dunia moja,” alisema Obama akijibu barua ya Eva.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya
ya Iringa alisema kwa kupitia Eva jamii ya watu Mlowa, Tanzania na Dunia kwa
ujumla inaweza kubadilika kwa kasi kubwa na kasisitiza wajibu wa viongozi katika
kutekeleza wajibu wao na umuhimu wa kuwandaa vijana mapema ili wawe viongozi wa
sasa na kesho watakaoshirikiana na wadau wengine kutimiza ndoto za watu wengi.
Kasesera alisema ni bahati na jambo la
kujivunia kwa binti huyo wa kijijini sauti yake kusikika hadi kwa Rais Obama na
kujibiwa kupitia mkutano mkubwa unaohudhuriwa na viongozi wa mataifa yote
dunia.
“Ni binti ambaye tayari yupo kwenye
kumbukumbu za Rais Obama. Ni wajibu wetu sasa kumuombea kwa Rais Dk Magufuli
ili atakapokuwa anakwenda kikazi nchini Marekani basi aongozane naye ili
akakutane na rais huyo uso kwa uso,” Kasesera alisema na baadaye kuungana na viongozi wengine kusaini
karatasi maalumu zenye wito wa Eva kwa viongozi na watendaji wa serikali.
Awali Mratibu wa Mradi wa Kijana Wajibika,
Oscar Kimaro alisema kwa kupitia mradi huo Restless Development wana lengo la kuwajengea
uwezo vijana ili waweze kuwaraia wema, kupaza sauti zao na kuwawezesha kuwa chachu
ya utawala bora kwa kukuza uwajibikaji wa viongozi na watendaji waserikali.
0 comments:
Post a Comment