Tuesday, 2 February 2016

MIUNDOMBINU MIBOVU HIFADHI YA MLIMA RUNGWE YAUKOSESHA WATALII


SERIKALI imetakiwa kujenga na kuimarisha barabara yenye urefu wa kilomita nne kutoka Kijiji cha Kyimo juu katika barabara kuu ya Mbeya Malawi kuelekea katika Hifadhi ya Mlima Rungwe katika kijiji cha Syukula wilayani Rungwe mkoani Mbeya ili kuongeza idadi ya watalii.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Muongoza watalii wa hifadhi hiyo, Mazao Fungo alipokuwa akizungumza na wanahabari wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzani (TAJATI) waliotembelea hifadhi hiyo kwa ufadhili wa WCS.

Fungo alisema katika hifadhi hiyo, idadi ya watalii haiongezeki moja ya sababu ikiwa ni miundombinu mibovu ya barabara kuelekea katika kijiji cha Syukula ambako kuna geti la kuingia hifadhini.

Alisema hifadhi hiyo imekuwa ikipokea wastani wa watalii 200 kwa mwaka pamoja na udogo wa gharama za kuingia hifadhini ambazo ni Sh 3000 kwa watanzania na dola 10 kwa wageni toka nje ya nchi.

Mhifadhi Mkuu wa Msitu wa Hifadhi Mazingira Hai Rungwe (TFS), Innocent Lupembe alisema mbali na kutokuwa na barabara ya kufika getini, kutotangazwa kwa hifadhi hiyo ni sababu nyingine ya kukosa idadi kubwa ya watalii wanaoitembelea.

Alisema Mlima Rungwe una vivutio vingi ambavyo havipatikani popote duniani lakini havijulikani kutokana na kutotangazwa vizuri ndani na nje ya nchi.

Alisema katika mlima Rungwe kuna Nyani adimu duniani anayepatikana katika mlima huo pekee anayejulikana kwa jina la Kipunji ambae aligunduliwa na Shirika la Uhifadhi mazingira (WCS) mwaka 2004.

Vivutio vingine  vilivyopo katika mlima huo ni pamoja na uoto wa asili uliojaa misitu iliyofunga, ukanda wa nyasi, ukanda wa mianzi na misitu yenye uwazi, Kreta pamoja na wanyama wengine kama Ngedere, Mbega, Nguruwe pori na Mbawala.


Ili iweze kufikika kirahisi, TFS kwa ufadhili wa Global Environmental Facility, United Nation Development Program na Wildlife Conservation Society ina mpango wa kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe. 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment