Monday, 29 February 2016

MAJALIWA AMSIMAMISHA KAZI DAKTARI ALIYEOMBA RUSHWA YA SH 100,000

mtw7

mtw6

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa Dkt. Fortunatus Namahala wa Kitengo cha Upasuaji katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula baada ya kutuhumiwa kudai rushwa ya Sh 100,000 ili aweze kutoa huduma.

Majaliwa pia ameagiza kufungwa kwa maduka yote ya dawa yaliyo nje ya hospitali hiyo kuanzia leo na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa huo, Alfred Luanda asimamie zoezi hilo mara moja.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo kwenye kikao cha watumishi wa hospitali hiyo alichokiitisha baada ya kutembelea maeneo kadhaa ya hospitali hiyo na kupokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa na ndugu wenye wagonjwa waliolazwa.

Mara baada ya kuwasili, Waziri Mkuu aliamua kwenda mojamoja mapokezi badala ya wodini kama alivyopangiwa na kuhoji ni kwa nini kuna dirisha moja la kupokelea wagonjwa wote.

“Dirisha la wazee lipo?,”  alihoji na kujibiwa kuwa hakuna. “Dirisha la wa watu wa Bima ya Afya (NHIF) lipo?,” alizidi kuhoji na kujibiwa kuwa halipo pia.

Majaliwa pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Shaibu Maarifa kuhakikisha anatenga dirisha maalum la wazee na sio kuwaacha wakisukumana na wagonjwa vijana.

Akiwa njiani kuelekea wodi aliyopangiwa kuiona, Waziri Mkuu alikutana na kundi la wagonjwa waliokuwa wakiimba “tuna jambo, tuna jambo” wakiashiria kutaka kusikilizwa.

Kati ya wauguzaji watatu aliowasikiliza, Waziri Mkuu alipokea kero mbalimbali ikiwemo kuuziwa dawa kwa bei za juu kwenye maduka ya dawa binafsi, lugha mbaya za madaktari na wauguzi, uchafu wa vyoo na uhaba wa maji.

Lakini ni kero ya Tatu Abdallah ndiyo iliyomgusa zaidi Waziri Mkuu baada ya kumueleza kuwa alilazimika kuuza shamba la baba yake la Ekari 2.5 ili apate fedha za kulipa gharama za kufanya upasuaji kwenye hospitali binafsi baada ya baba huyo kutimuliwa kutoka hospitali ya Ligula.

Akielezea zaidi, Tatu amesema; “ Februari 1, mwaka huu nilimleta baba yangu hapa nikaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji. Nikaandikiwa ninunuue dawa za Shilingi 85,000 hapo nje (pharmacy haikumbuki jina) pia uzi wa kushonea kwa Shilingi 25,000 na baada ya kununu vyote hivyo, daktari akasema anataka Sh 100,000 ya kwake ili aweze kufanya zoezi hilo  lakini hadi Februari 7, baba hakuwa amefanyiwa upasuaji huo.”

“Februari 12,  baba alitolewa wodini na kuambiwa arudi tarehe Februari 16. Niliumia kwasababu kijiji tunachotoka ni mbali na hali ya baba ilizidi kuzorota. Ndipo baba akaniambia nirudi kijijini kwetu Kilomba nikauze Ekari 2.5 za shamba lake ili tulipie matibabu. Niliuza na kumpeleka baba katika zahanati ya Sajora. Huko nililipa Shilingi 560,000 na baba akafanyiwa upasuaji na sasa hivi yuko nyumbani,” aliongeza.

Akiwa katika kikao na watumishi hao, Waziri Mkuu aliwainua madaktari wote ili wajitambulishe ndipo akamuomba mama aliyedaiwa rushwa aende kumshika mkono daktari mhusika.

Baada ya mama huyo kumtambua daktari huyo, Waziri Mkuu alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na Katibu Tawala wa Mkoa kushirikiana na TAKUKURU kufanya uchunguzi wa jambo hilo hadi mwisho na hatua zingine stahiki ziweze kuchukuliwa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment