Monday, 1 February 2016

LUBUVA ASEMA DK MAGUFULI HAWEZI KUINGILIA MAAMUZI YA TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR

jaji lubuva

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Jaji Damian Lubuva amemhakikishia Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa tume hiyo ipo huru na haijawahi kuingiliwa kimaamuzi na Rais wala kiongozi yoyote.

Jaji Lubuva amesema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli ambapo alikuwa akimpa taarifa juu ya yaliyojiri katika kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika Mjini Kampala, Uganda na kujadili kuhusu uchaguzi Mkuu wa Uganda unaotarajiwa kufanyika tarehe 18 mwezi huu.

Amesema katika kikao hicho ambacho yeye alikuwa mwenyekiti, wamezungumzia umuhimu wa tume ya uchaguzi kuwa huru huku wakichukulia mfano wa Tanzania ambayo imetoka katika uchaguzi mkuu miezi michache iliyopita.

Jaji Lubuva amesema pia watu wanaosema Rais anapaswa kuingilia kati masuala ya uchaguzi iwe Tanzania bara ama Zanzibar wanafanya makosa, kwani kwa namna yoyote Rais hana mamlaka hayo na hivyo hawezi kuingilia maamuzi ya tume hizo.


Jaji Lubuva amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kikatiba hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar na hata huku bara pia hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya tume.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment