Saturday, 27 February 2016

COSATO CHUMI AKUSANYA CHANGAMOTO ZA WADAU WA MAENDELEO JIMBONI KWAKE MAFINGA MJINIMBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi(CCM) amewatembelea wadau mbalimbali wa jimbo hilo na kuchukua changamoto zao atakazoanza kuziwasilisha katika kikao cha bunge lijalo na mamlaka zingine zinazohusika.

Chumi ambaye ni mbunge wa jimbo hilo jipya liliundwa kutoka katika majimbo ya Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini mkoani Iringa alisema ameitumia pia ziara hiyo kufahamiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wa jimbo hilo.

Katika ziara hiyo aliyoifanya kwa zaidi ya wiki moja, mbunge huyo alitembelea makampuni mbalimbali ikiwemo Kiwanda cha Sao Hill, Msitu wa Taifa wa Sao Hill, kiwanda cha Pareto na kampuni ya Simu ya TTCL.

Wengine waliotembelea ni pamoja na Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), NSSF, Benki ya Wananchi Mudfindi (Mucoba), NMB benki na CRDB Benki.

“Baada ya kutembelea taasisi hizo; natarajia pia kutembelea magereza, vituo vya kutolea huduma za afya, taasisi za elimu na taasisi nyingine za umma na binafsi wakiwemo wajasiriamali wadogo na wakubwa, machinga na wengine,” alisema.

Akiwa katika kiwanda cha SaoHill kinachomilikiwa na kampuni ya Green Resources Ltd (GRL) inayojishughulisha na upandaji miti wilayani Mufindi na Kilombero, Chumi alipokea changamoto mbalimbali za kibiashara zinazohusu kampuni hiyo.

 Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Roselyn Mariki alisema kampuni yao ina uwezo wa kuzalisha na kuuza sehemu kubwa ya nguzo zinazohitajika na shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) endapo wataongezewa mgao wa kuvuna miti katika shamba la Msitu wa Taifa wa Saohill ambao pia upo wilayani Mufindi.

Mariki alisema kwasasa kampuni yao inauwezo wa kuzalisha na kuuza Tanesco nguzo 90,000 tu kwasababu ya changamoto ya uvunaji wanayopata katika msitu huo.  

Alisema kwa sasa wanapata mgao wa kuvuna meta za ujazo 120,000 za miti kwa mwaka; kiasi ambacho si chote kinakuwa na miti inayofaa kwa ajili ya nguzo hizo.

Mkurugenzi huyo aliomba Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kupitia Msitu wa Taifa wa Saohill wapewe leseni ya uvunaji miti kwa mfumo wa kuvuna ile inayofaa kwa nguzo na na ile inayofaa kwa matumizi mengine wauziwe wadau wengine ili waweze kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ya kuzalisha nguzo hizo nchini badala ya kuendelea kuagiza kutoka Afrika Kusini ili kukidhi mahitaji yake.

Pamoja na ombi lao hilo, Mariki alizungumzia ucheleweshaji wa malipo ya nguzo wanazoziuza Tanesco ambazo pia huchelewa kuchukuliwa pamoja na kuandaliwa mapema kwa kuzingatia mkataba.

Kuhusu samani, Mariki alisema wamepokea kwa mikono miwili agizo la Mhe Rais John Magufuli linazozitaka taasisi za umma kuacha kuagiza samani kutoka nje na kununua kutoka kwa wazalishaji wa ndani, kikiwemo kiwanda chao cha Sao Hill ambao ni wazalishaji wa samani bora na vifaa vingine vitokavyo na mbao.

Wakati huo huo, Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) imesema nishati ya umeme inavyokatika mara kwa mara inaathiri uzalishaji na hatimaye kuwaongezea gharama na kuwakosesha mapato wao pamoja na serikali inayokusanya kwa njia ya kodi.


Kaimu Meneja Mkuu William Kufakwepasi aliomba Tanesco ifunge laini madhubuti za umeme na ujenge kituo kidogo cha kusambazia umeme katika mji huo wa Mafinga ambao umekuwa ukipata nishati hiyo kutoka Mgogolo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment