Thursday, 4 February 2016

CHENGE AMUADHIBU MKE WA KAFULILA, NI MBUNGE WA VITI MAALUMU CHADEMA

kafulila

Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jesca Kishoa amesimamishwa kuhudhuria vikao viwili vya bunge baada ya kushindwa kuwasilisha ushahidi juu ya tuhuma alizozitoa katika bunge hilo kwamba Waziri Dk Harrison Mwakyembe anahusika na kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki.

Mapema wiki hii, Kishoa  ambaye ni mke wa aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alisema Dk Mwakyembe alihusika kununua mabehewa feki 274 jambo ambalo lilizua mjadala mkali na bunge kumtaka mbunge huyo atoe ushahidi ndani ya siku 3.

Katika mkutano wa leo, mwenyekiti wa bunge Andrew Chenge amelikumbusha bunge kuhusiana na kauli ya Kishoa na kusema kuwa mbunge huyo alitakiwa kwa mujibu wa kanuni za bunge kanuni ya 63(6) atoe ushahidi kwa ofisi ya bunge na ndani ya siku zote ofisi ya bunge haijapata ushahidi huo.

Kutokana na Mbunge huyo kushindwa kutekeleza maamuzi ya bunge, mwenyekiti wa bunge amemtaka kufuta kauli yake na mbunge huyo akakaidi ndipo Mwenyekiti akamuamuru atoke nje mara moja na kwamba hataruhusiwa kuhudhuria vikao vya bunge kwa siku mbili zilizobakia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment