Tuesday, 23 February 2016

CCM YAKANUSHA KUFUTWA KWA KESI YA MWAKALEBELA DHIDI YA MCHUNGAJI MSIGWA


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema kesi ya kupinga matokeo iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wake ubunge jimbo la Iringa Mjini, Frederick Mwakalebela iko pale pale, kikipinga taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana na kuchapwa katika baadhi ya magazeti leo kwamba kesi hiyo imefutwa.

Akizungumza na wanahabari hii leo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema; “kwa mambo yanayohusu sheria ni kawaida sana hata kwa wanasheria wenyewe kufanya makosa ya kiufundi.”

Mtenga alisema katika shauri lao la awali ambalo wanalifanyia marekebisho hawakumuingiza mwanasheria mkuu wa serikali katika orodha ya wanaoshitakiwa.

“Tumewaiteni wanahabari tuwaambieni kwamba Msigwa hajashinda kesi. Kesi ipo na tungependa wananchi wajue kwamba kesi ya msingi ipo na inaendelea,” alisema.

Alisema; “Msigwa hawezi kushinda kesi kwenye FaceBook, wala kwenye magazeti, kwa mujibu wa sheria atashinda kesi hizo pale tu ambapo mahakama itatimiza wajibu wake kwa kutoa haki.”

Naye Mwakalebela alisema shauri lake la kupinga ushindi wa Mchungaji Msigwa limekuwa likipata mapingamizi mengi.

“Pingamizi lingine ni baada ya mwanasheria wangu kutomuweka mwanasheria mkuu wa serikali na hivyo maahakam kuliondoa ili likarekebishwe,” alisema.

Kuondolewa kwa shauri hilo mahakamani haina maana kwamba limefutwa kama ilivyotasfiriwa na upande wa pilia na ndio maana mahakama hiyo hiyo imewapa fursa ya kulirudisha tena mahakamani.

“Kwa sasa wanasheria wetu wanalifanyia kazi hilo vizuri ili litakaporudi mahakamani kusiwepo na dosari zingine na badala yake lianze kusikilizwa,” alisema.

Alisema kesi hiyo ya kupinga matokeo itamalizwa kwa pande zote kusikilizwa ili haki itendeke na sio kwa maamuzi ya propaganda.


Katika shauri la msingi la kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo, Mwakalebela aliwatuhumu Mchungaji Peter Msigwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Iringa Mjini, Ahmed Sawa kwa kukiuka sheria na taratibu za uchaguzi hali iliyopelekea yeye kupata matokeo mabaya yasiyo halali.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment