Tuesday, 2 February 2016

BODI YA REA KUWAFYEKA WAKANDARASI WALIOSHINDWA KUKAMILISHA MIRADI YA UMEME VIJIJINI


BODI ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetangaza kuwanyima kazi wakandarasi wake wote ambao kwasababu zilizo ndani ya uwezo wao wameshindwa kukamilisha miradi ya kusambaza umeme vijijini awamu ya pili.

Bila kutaja idadi ya wakandarasi wanaofanya nao kazi katika awamu hiyo ya pili inayotarajia kukamilika Machi 30 mwaka huu, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Edmund Mkwawa alisema:

“Tunaingia awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi huu wa umeme vijijini, kwahiyo tutakuwa makini sana, hatutawafikiria kabisa wakandarasi ambao kwa uzembe wao wameshindwa kukamilisha kazi walizopewa ndani ya muda uliopangwa katika awamu ya pili.

Alisema azma hiyo inayolenga kuongeza ufanisi katika usambazaji wa umeme vijijini haitawahusu wakandarasi ambao kwasababu zilizo nje ya uwezo wao.

Aliwataja baadhi ya wakandarasi ambao wamechelewa kukamilisha miradi waliyopewa kuwa ni pamoja na Sinotec inayofanya kazi Mbeya Vijijini, Mbozi, Chunya, Sumbawanga Vijiji na Nkasi.

Wengine ni Spencon (Singida na Kilimanjaro), CHICCO-CC Joint venture (Mwanza na Tabora), CCC-Nigeria (Manyara), MBH Power Ltd (Morogoro, Pwani na Lindi) na LYL Power Ltd wanaofanya kazi katika mikoa ya Ruvuma na Shinyanga.

Mkwawa alitoa taarifa hiyo alipokuwa akizungumza na wanahabari mjini Iringa mara baada ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme vijijini katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma.

Miradi hiyo inatekelezwa na serikali kupitia ufadhili wa Mfuko wa Nishati Vijijini (REF) unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akizungumzia maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo awamu ya pili, Mkwawa alisema; “utekelezaji unaendelea na hadi sasa umefikia asilimia 85.”

Alisema matayarisho ya mradi kabambe awamu ya tatu utakaotekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 yameanza na kwamba kazi zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa njia za usambazaji wa umeme wa msongo wa 11kV na 33kV zenye urefu wa kilometa 25,000 na ujenzi wa njisa za usambazaji umeme za msongo wa 0.4kV na 023kV zenye jumla ya kilometa 38,000.


Alisema katika awamu hiyo wateja wapya 340,000 wataunganishwa na nishati hiyo kupitia awamu hiyo ya tatu itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha ujao kwa gharama ya zaidi ya Sh Bilioni 2,930.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment