Sunday, 21 February 2016

BAADA YA LUWAVI KUWATEMBELEA WAHANGA WA MAFURIKO IRINGA, KESHO ANAKUJA WAZIRI MKUU


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, kesho Jumatatu anatarajia kuzitembelea kaya zaidi ya 145 zilizoathiriwa na mafuriko katika kata ya Pawaga, wilayani Iringa kwa lengo la kuzifariji ikiwa ni siku mbili tu toka Naibu Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rajab Luwavi afanye hivyo.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuu anatarajiwa kuambatana na Mbunge wa Jimbo la Isimani ilipo kata hiyo, William Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; ambao kwa pamoja watajionea hali halisi ya maisha ya kaya hizo zinazoendelea kusaidiwa ili zirudi katika maisha yao ya kawaida.

Akiwa katika kambi za muda za wahanga hao katika vijiji vya Itunundu na Kimande juzi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM alikabidhi kwa niaba ya chama chake msaada wa mifuko 80 ya sembe kwa walengwa hao.

Mbali na msaada huo jana, Umoja wa Wanawake (UWT) wilaya ya Iringa kwa kushirikiana na Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Iringa, Rose Tweve (CCM) nao ulitoa vitu mbalimbali kwa wahanga hao vikiwemo vitenge doti 70, sabuni, nguo za ndani na nguo za watoto.

Akikabidhi msaada huo, Luwavi aliwapongeza wale wote waliohusika kuhakikisha hakuna kifo kilichotekea miongoni mwa watu waliokumbwa na mafuriko baada ya kuzingirwa na maji katika kata hiyo.

Akitoa taarifa ya mafuriko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesera alisema; “serikali kwa msaada wa wadau wake na Jeshi la Wananchi Tanzania wameanza ujenzi wa majengo mawili makubwa yatakayotumika na baadhi ya kaya hizo kama makazi ya muda kabla hawajahamia katika majengo yao.”

Huku Luwavi akiagiza majengo hayo yatumike kutolea elimu baada ya wahanga hao kuondoka, Kasesera alisema serikali itaratibu mpango wa kufyatua tofali za bloku zitakazokopeshwa kwa wahathirika hao kwa ajili ya ujenzi wa nyumba zao katika viwanja watakavyopewa.

Alisema tofali hizo zitakopeshwa kwa sharti nafuu la kuzilipia baada ya familia hizo kuanza uzalishaji na uuzaji wa uuzaji wa mazao yao wanayolima ukiwemo mpunga na mahindi.

“Pamoja na ofa hiyo kubwa, serikali itatoa bati 20 kwa kila mhanga kati ya wahanga 10 wa kwanza watakaokuwa wa kwanza kujenga nyumba zao,” alisema.

Akizungumzia jinsi serikali ilivyojipanga kuboresha miundombinu katika maeneo mapya yaliyotengwa kwa ajili ya wahanga hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka alisema upimaji wa viwanja katika maeneo hayo unaendelea.

Alisema pamoja upimaji huo, serikali kwa kushirikiana na wadau wake itahakikisha inaboresha huduma zingine za jamii ikiwemo ujenzi wa visima 19 vya maji safi na salama katika maeneo yote yatakayokaliwa na waathirika.

“Pia tutajikita kuangalia suala zima la ujenzi wa vyoo bora, tutawahamisha watu walioingia katika eneo la Nyalu ambalo ni eneo la hifadhi ya jamii ambalo watu hawatakiwi kuishi ili kuwaondoa katika hatari ya mafuriko,” alisema.


Ili kufanikisha ujenzi wa vyoo bora, Luwavi alimuagiza Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga kuwatumia vijana wa chama hicho kuifanya kazi ya kuchimba mashimo ya vyoo hivyo kwa kujitolea kama muendelezo wa mchango wa chama hicho kwa wahanga hao. 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment