Thursday, 11 February 2016

ASASI ZA KIRAIA MIKOA YA KUSINI ZAIPASHA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI


IKIWA imepita miezi zaidi ya mitatu tangu ufanyike Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani nchini, asasi za kiraia za mikoa ya Nyanda za Juu Kusini zimetoa ya moyoni katika mkutano wa tathimini ya elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi huo.

Katika mkutano huo uliofanyika mjini Iringa jana baina ya asasi hizo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), baadhi ya asasi hizo zimesema pamoja na kwamba uchaguzi huo ulimalizika kwa kile kinachoonekana katika mazingira yaliyokuwa salama; ni lazima ieleweka kwamba zilikuwepo changamoto mbalimbali zinazotakiwa kufanyiwa kazi na tume hiyo.

“kwahiyo sio sahihi sana kuendelea kusikia kutoka wa watu mbalimbali wakiisifia tu tume hiyo ni lazima tuziseme dosari za msingi zilizojitokeza ili ziweze kufanyiwa kazi katika chaguzi zijazo,” alisema mwakilishi wa asasi ya Wazee ya mjini Iringa, Bathlowmeo Kuzungula.

Mwakilishi wa Chama cha Wasioona Mkoani Iringa, Steven Changara kwa upande wake alisema dhana ya kura ya siri kwa kundi la watu wasioona katika uchaguzi huo haikufanikiwa kwani mbali na kutopata elimu, vifaa vya kupigia kura kwa ajili yao havikuwa na ubora jambo lililowalazimu kutumia wasaidizi kupiga kura zao.

Naye John Ndumbalo wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Iringa alisema katika maeneo mengi kulikuwepo na hisia ya uchakachuaji matokeo kwasababu matokeo ya kura yalichelewa kutolewa na akaiomba tume hiyo ijitahidi kwa siku za usoni kutoa matokeo hayo ikiwezekana ndani ya saa 48.

Katibu Mtendaji wa Klabu ya Waandishi Mkoa wa Iringa (IPC) Tukusiwga Mwaisumbe alisema tume na wadau wa uchaguzi wanapaswa kushirikiana bila ubaguzi wowote na vyombo vyote vya habari ili elimu ya mpiga sahihi iweze kuwafikia wapiga kura wengi zaidi.

Naye Meristela Mapunda wa Songea alisema kulikuwepo na utata katika kuliboresha daftari la wapiga kura huku baadhi ya wapiga kura wakijiandikisha katika maeneo ambayo si makazi yao rasmi na katika maeneo mengine vifaa vya kupigia kura vilichelewa kufika vituoni.

Akifungua mkutano huo, Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC), Mchanga Hassan Mjaa alisema sheria ya Taifa ya Uchaguzi Na 1 ya mwaka 1985 (sura 343) kifungu cha 4C inaipa NEC jukumu la kisheria la kutoa elimu ya mpiga kura na kusimamia asasi, makundi au watu wanaotoa elimu hiyo.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana jumla ya asasi za kirai 451 ziliomba kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura, kati ya hizo ni asasi za kiraia 447 zilizopewa kibali kwa ajili ya kufanya kazi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Asasi hizo zilikuwa na jukumu la kuhamasisha na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kushiriki na kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na hatimaye kushiriki katika uchaguzi huo,” alisema.

Alisema Tume inaangalia uwezekano wa kuishauri serikali pamoja na mashirika ya kimataifa hapo baade waone uwezekano wa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuzifadhili asasi za kirai ili ziweze kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi wengi zaidi hasa wa vijijini.

Akizungumzia changamoto zilizotolewa na wawakilishi wa asasi hizo kamishina huyo alisema amezichukua na zitafanyiwa kazi kwa kuzingatia mazingira na sheria za nchi.

“Licha ya changamoto hizo na zingine Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa wa mafanikio makubwa ukilinganisha na Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment