Monday, 1 February 2016

AKAMATWA JIJINI DAR ES SALAAM AKIUZA BASTOLA KAMA PIPI


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja raia wa Malawi (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama) kwa kosa la kuuza bastola ikiwa na risasi zake 10 bila ya kuwa na vibali halali vya vinavyomruhusu kufanya biashara hiyo .

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema jeshi hilo lilimtia nguvuni raia huyo Januari 29 mwaka huu akiwa na bastola hiyo aliyokuwa akiiuza maeneo ya Sinza Manispaa ya Kinondoni.

Alisema kwa kushirikiana na nchi ya Malawi pamoja na vikosi vya usalama vya Interpol Jeshi la Polisi linafuatilia kwa karibu taarifa za raia huyo ilikuangalia kama ana rekodi zozote za uhalifu.

“Tunaendelea kumchunguza ilitujue ameshawahi kuuza silaha ngapi nchini ili tujue jinsi gani ya kumbana awataje aliowauzia na jeshi la polisi liwatie nguvuni na hatimaye kuwapokonya silaha hizo ili zisije kutumika katika matukio ya kihalifu,”alisema Kamanda Sirro

Katika hatua nyingine Jeshi hilo linamshikilia Hassan Ziko (38) kwa tuhuma za wizi wa gari lenye namba za usajili T335 BEQ Toyota Hiace lenye rangi ya kijani na wengine watatu waliokamatwa na gari la uwizi aina ya Suzuki Carry yenye namba za usajili T 435 BVM huko mbeya.

Kamanda Sirro alisema kuwa Jeshi hilo lilimtia nguvuni mtuhumiwa wa kwanza Ziko ambaye ni mkazi wa Nzasa B kata ya Chanika ambapo baada ya mahojiano mtuhumiwa alikiri kuuziwa gari hiyo na kijana mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Aziz.

Aliongeza kuwa upelelezi ulifanyika na ikagundulika kuwa gari hiyo iliibiwa Septemba 9 mwaka 2015 maeneo ya Lumumba na Uhuru City Centre jijini Dar es Salaam kwenye maegesho ya magari ambapo gari hilo ilikuwa na namba zake za awali ambazo ni T 133 DCT.

Alisema kuwa watuhumiwa wengine watatu ambao majina yao yanafichwa kwa sababu za kiusalama Januari 23 mwaka huu walikamatwa na gari aina ya Suzuki Carry walioiba jijini Dar es Salaam na kuipeleka mkoani Mbeya.

“Katika tukio hilo tumekamata watuhumiwa watatu ambao wamehusika na wizi huo uliotokea Disemba 20 mwaka 2015 huko maeneo ya Tandale baada ya watu hao kumdanganya dereva wa gari hiyo walikuwa na mzigo wa kubeba kutoka hapo na baada ya dereva kushuka mmoja wao alikimbia na gari hiyo,”alisema Kamanda Sirro.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment