Sunday, 3 January 2016

WAZIRI MKUU AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI RUVUMA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo anatarajia kutua wilayani Songea Mkoani Ruvuma katika ziara yake ya kikazi itakayomuwezesha kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo.

Majaliwa anaifanya ziara hiyo mkoani Ruvuma ikiwa ni siku chache baada ya kumaliza ziara yake mkoani Kigoma.

Mkuu wa Mkoa, Said Mwambungu amesema Waziri Mkuu atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Songea saa 6 mchana, ambapo atapokelewa na viongozi wa serikali na vyama vya siasa, kisha atakwenda moja kwa moja Ikulu Ndogo na kusomewa taarifa ya mkoa.

Kesho asubuhi Waziri Mkuu atafungua Benki ya Posta Tawi la Songea na kutembelea Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea kabla ya kuzungumza na wafanyakazi wa hospitali hiyo. Pia Waziri Mkuu atazungumza na watumishi wa idara zote za serikali waliopo mjini Songea.

Baada ya kumaliza kuzungumza na watumishi hao, atatembelea Kitengo cha Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) na kukagua maghala yanayotumika kwa ajili ya kuhifadhi chakula.

Waziri Mkuu pia atatembelea ujenzi wa makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Songea katika kijiji cha Lundusi kata ya Maposeni na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.

Mwambungu amewaomba  wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ambayo Waziri Mkuu atatembelea, ikiwemo barabarani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment