Wednesday, 13 January 2016

WALIOTUHUMIWA KUTAKA KUTAPELI MATREKTA YA WAKULIMA WA TUMBAKU WACHUNGUZWA KABLA YA KUFIKISHWA MAHAKAMANI


WIKI moja imepita bila mafanikio tangu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvivu, Mwigulu Nchemba amuagize Mwenyekiti wa Kampuni ya Umoja wa Wakulima wa Tumbaku Iringa (ITCOJE Ltd), Msafiri Pamagila pamoja na viongozi wengine nane wa vyama vya ushirika vya msingi vya zao hilo kuachia ngazi na kukabidhi ofisi za vyama hivyo pamoja na mali zote wanazozisimamia.  

Viongozi hao akiwemo pia Afisa Ushirika wa Wilaya ya Iringa, Emanuel Samile walituhumiwa katika kikao baina ya waziri huyo na wakulima wa zao hilo, kujimilikisha kinyemela matrekta tisa yaliyokopeshwa kwa vyama hivyo miaka minne iliyopita kupitia mkopo uliotolewa na benki ya CRDB.

Katika kikao hicho cha Januari 5 mwaka huu, Nchemba aliagiza viongozi hao wakabidhi ofisi, matrekta hayo na mali zingine za vyama hivyo siku iliyofuata mara tu baada ya kuondoka mkoani Iringa, maagizo ambayo mpaka jana yalikuwa hayajatekelezwa.

Pamoja na kuwataka viongozi hao waachie ngazi na taratibu za kujaza nafasi zao zifanywe haraka iwezekanavyo, Waziri Nchemba alimuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Lutabazibwa kuifuta bodi ya ITCOJE na kuhakikisha taratibu za kuunda bodi mpya zinafanywa haraka kwa kadri itakavyowezekana.

Mbali na kumiliki gari la kisasa aina ya Toyota Land Cruiser VX bodi hiyo pia inamiliki roli aina ya Scania linalodaiwa kufanya kazi ya kusambaza kuni na pembejeo kwa wanachama wa vyama hivyo na kazi zingine za usafirishaji ambazo mapato na matumizi yake hayako wazi.

Akizungumza na HabariLeo jana, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera ambaye ni mmoja wa viongozi wa serikali mkoani hapa waliopewa jukumu na waziri huyo la kusimamia maagizo yake hayo, alisema:

“Baada ya maagizo yale tulishauriana na Waziri na kuamua kuunda timu itakayofanya uchunguzi wa kina wa tuhuma zote dhidi ya viongozi hao ili watakaobainika wasiishie kufukuzwa tu katika nafasi zao lakini pia wafikishwe katika vyombo vya dola.

Kasesera alisema timu hiyo inayoshirikisha watu wataalamu wanne kutoka ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Bodi ya Tumbaku Tanzania, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa ilipewa siku saba iwe imekamilisha kazi hiyo.

“Mpaka jana ilikuwa ni siku ya tano na kazi hiyo ilikuwa bado haijakamilika; nimeongea na waziri na nimemuomba tuongeze siku nyingine saba ili timu hiyo ikamilishe kazi yake kwa ufanisi,” alisema.

Alisema lengo la kuunda timu hiyo ni kusaidia kupata matokeo yatakayowezesha maamuzi yatakayochukuliwa dhidi ya viongozi watakaobainika na tuhuma mbalimbali katika vyama hivyo yasiwe na mgongano wa kisheria.

Awali katika kikao chao na waziri huyo ilielezwa kwamba viongozi hao kutoka chama cha ushirika Mfyome, Magubike, Kiwemu, Kitai, Mhanga na ITCOJE  yenyewe walimiliki matrekta hayo kwa utetezi kwamba ni baada ya wanachama wa vyama hivyo kutoa ridhaa hiyo ikiwa ni motisha kwa kukubali kuwa wasimamizi wake mpaka mikopo yake itakapokwisha.


Taarifa iliyotolewa kwa waziri huyo na Mkurugenzi wa CRDB tawi la Iringa, Kisa Samwel inaonesha matrekta hayo yanayoendelea kutumiwa kama dhamana ya mikopo ya vyama hivyo kwa msimu wa kilimo wa 2015/2016, yalikwishalipiwa mikopo yake yote na vyama hivyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment