Tuesday, 19 January 2016

WALIOFUNGA BARABARA JIJINI DAR ES SALAAM WATIWA MBARONI

bomoabomoa

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia wananchi kadhaa, wakituhumiwa kufanya fujo na kufunga barabara ya Kawawa kwa muda na kuchoma matairi.

Kukamatwa kwa watu hao, wanaosadikiwa ni wa Bonde la Mkwajuni jijini Dar es Salaam, kunatokana na kile kilichodaiwa ni kufunga barabara baada ya maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuweka alama ya X katika vibanda walivyojenga watu hao kwa ajili ya makazi.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Simoni Sirro alisema wakazi hao watahojiwa kueleza sababu za kufunga barabara hizo na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano.

Vurugu hizo zilizotokea jana saa 6 mchana, inadaiwa zilisababishwa na baadhi ya vijana wanaoishi katika maeneo hayo, ambao walichoma matairi pande zote za barabara na kusababisha foleni na usumbufu kwa watumiaji. Polisi na gari la zimamoto lilifika eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo na wananchi wengine.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment