Saturday, 16 January 2016

SERIKALI YAWASHUGHULIKIA VIGOGO WATATU MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA


Serikali kupitia  Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano  Prof.Makame Mabarawa  imemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Charles Chacha na kutaka kuhamishwa mara moja kwa Mhasibu Mkuu Alhaji Said Mteule na Meneja manunuzi wa taasisi hiyo, Said Kaswela kwa kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya taasisi.

Mbarawa alitoa agizo hilo jana akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango pamoja na watendaji wa TCAA katika ziara aliyoizungumzia kuwa ni ya kuangalia uendeshaji na ukusanyaji wa mapato unavyofanyika katika taasisi hiyo.

Pamoja na maamuzi hayo, serikali imeona pia ifanye uchunguzi kuhusu ununuzi wa mtambo wa kufuatilia vyombo angani unaojulikana kama Automatic Data Surveillance-Broadcast (ADS-B) na mtambo wa kukusanya taarifa za usafiri wa anga (AMHS), ambayo imegharimu kiasi cha Euro milioni 1.5.

Mitambo hiyo ilitakiwa kuanza kufanya kazi tangu Novemba mwaka jana, lakini mpaka sasa haijaanza kufanya kazi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mpango  alisema kikubwa kinachopiganiwa na serikali ni kukusanya mapato yote ya kodi na yasiyo ya kodi na katika mamlaka hiyo, kuna vyanzo vinavyoweza kuiingizia serikali fedha nyingi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment