Thursday, 7 January 2016

SERIKALI YAGOMEA VIWANGO VYA NAULI YA MABASI YAENDAYO KASI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haijaridhia viwango vipya vya nauli ya mabasi yaendayo kasi vilivyopendekezwa na waendeshaji wa huduma ya mabasi yaendayo kasi Dar es salaam (UDART).

Akizungumza  leo na waandishi  wa habari, mara baada ya kuwasili katika  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa  wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku 3, Waziri Mkuu amesema  Serikali haijaridhia viwango vipya vya nauli ya mabasi yaendayo kasi. Ambapo nauli ya kutoka Mbezi hadi Kimara shilingi 700, Mbezi hadi Kariakoo shilingi 1200, na nauli ya kutoka Mbezi hadi Mwenge shilingi 1400 na wanafunzi watatozwa nusu ya viwango hivyo vya nauli.

Waziri Mkuu amesema gharama hizi ni kubwa mno kwa wananchi na watumishi, mradi ulilenga kumrahisishia mtumishi wa Serikali anayeishi nje ya jiji, “Serikali iliwekeza katika mradi huu ili kusaidia watumishi na wananchi ambao hawana vipato vikubwa” alisema Waziri Mkuu.

Aidha, ameagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene  na  Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi, na Mawasiliano pamoja na wadau wakutane  kupanga upya  viwango hivyo na kama watashindwa basi Serikali  itaendesha mradi huo.     
      
Tarehe  25, Novemba 2015, Waziri Mkuu alimuagiza aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI na waendeshaji wa  mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es salaam (UDART) kupitia misuada yote na kurekebisha miundombinu  ili mradi huo wa mabasi uanze kufanya kazi ifikapo tarehe 10, Januari 2016, imebainika kwamba  UDART hawakuandaa mpango wa biashara  wala kuanisha gharama za uendeshaji.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,
11410 DAR ES SALAAM

JUMATANO, JANUARI 6, 2016.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment