Sunday, 3 January 2016

MCHUNGAJI MSIGWA KUWATAJA KWA MAGUFULI WAFANYABIASHARA WAKWEPA KODI IRINGAMBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ameungana na watanzania wengine kumpongeza Rais Dk John Magufuli kwa sera yake ya kutumbua majipu huku akiahidi kumtajia wafanyabiashara wakubwa wa mjini Iringa aliosema ni wanaokwepa kodi.

Akiwashukuru wapiga kura wa mjini hapa kwa kumchagua kwa mara nyingine tena kuwa mbunge wao na kuwachagua madiwani 14 kutoka Chadema kati ya madiwani 18 wanaounda halmashauri ya manispaa ya Iringa katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Mwembetogwa, mjini hapa Mchungaji Msigwa alisema:

“Katika kutumbua majipu tunamuunga mkono Dk Magufuli na niahidi tutamwonesha wafanyabiashara wakubwa wanaokwenda kodi.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na wabunge wa viti maalumu  wa chama hicho, Suzan Mgonakulima na Grace Tendega, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe na madiwani wote wa chama hicho, Mchungaji Msigwa alisema mbali na wafanyabiashara hao, baraza lao madiwani litahakiki taarifa za ulipaji kodi, hasa za majengo, zinazokihusu Chama cha Mapinduzi (CCM) mjini Iringa.

“Yapo madai yanayoonesha CCM hapa Iringa hailipi kodi za majengo yake mbalimbali. Majengo hayo ni pamoja na uwanja wa Samora, jengo la CCM Mkoa, vibanda vya biashara maarufu kama vibanda vya kitimoto na vingine vya maduka ya pombe, ofisi na uwanja wa sabasaba,” alisema.

Alisema watafanya uhakiki katika majengo hayo yote ili kujilidhisha kama ule uhalali wa serikali yao unaowawezesha kukusanya kodi kutoka kwa watu wengine, unatumika pia kukusanya kodi katika miradi yao mbalimbali inayotakiwa kulipiwa kodi.

Alisema ili waweze kufikia malengo ya kimaendeleo waliyojiwekea katika kipindi cha miaka mitano ijayo, baraza lao la madiwani limepanga kusimamia kwa nguvu zake zote ukusanyaji wa kodi kwa kuhakikisha wenye kingi wanalipa zaidi ya wale wenye kidogo.

Akizungumzia migogoro ya ardhi mjini Iringa, mbunge huyo alisema chanze chake ni ukosefu wa ardhi na akashauri wale wenye mashamba ndani ya manispaa wafanye utaratibu wa kuyakabidhi manispaa na walipwe fidia ili mashamba yao yapimwe viwanja vitakavyogaiwa kwa wananchi.

Akizungumzia mikakati ya halmashauri yake, Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe alisema halmashauri yake imepanga kuongeza makusanyo yake ya mwaka kutoka Sh Bilioni 2.5 za sasa hadi Sh Bilioni 7 katika kipindi cha 2016/2017.


Alisema halmashauri hiyo itahakikisha inakusanya kodi zake zote kikamilifu  na sehemu ya fedha zitakazopatikana zitatumika kununua gari la kubeba wagonjwa na kubeba taka ili kuboresha huduma katika sekta ya afya na usafi wa mazingira.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment