Thursday, 21 January 2016

MBEGU BORA KUNUSURU MAZAO YA MISITU KATIKA SOKO LA KIMATAIFA


WAKULIMA wa mazao ya misitu nchini wamehimizwa kutumia mbegu bora ili kukuza uzalishaji wa mazao hayo ambayo matumizi na soko lake linakuwa siku hadi siku.

Mbegu hizo ni zile zilizofanyiwa utafiti wa kina na kuzingatia kanuni bora za kilimo.

Mratibu wa fafunzo wa Taasisi ya Uendelezaji Misitu Tanzania (FDT) Hamis Malinga alisema pamoja na matumizi ya mbegu bora, wakulima wa mazai hayo wanatakiwa kuzingatia kanuni zote za kilimo chake ili kuleta matokeo tarajiwa.

Malinga alikuwa akizungumza na wawakilishi wa wakulima zaidi ya 120 kutoka mikoa a Iringa, Njombe na Ruvuma wa katika kijiji cha Kisolanza wilaya ya Iringa ambako kuna shamba la mfano la uzalishaji wa miti.

Alisema wakulima wakiyazingatia hayo, mazao yao yatamudu ushindani katika soko la dunia na hivyo kuwaongezea kipato kinachoweza kuwaondoa kabisa katika umasikini wa kipato na kuongeza makusanyo ya Taifa. 

Alisema upandaji miti kwa wakati na kwa kutumia mbegu bora, kuitunza kwa kupalilia na kuweka mbolea au dawa kama inavyotakiwa kunasababisha ukuaji wa haraka na uongeza uzalishaji.

“Ili tufikie lengo la kuzalisha mazo bora ya misitu ni muhimu tukashirikiana kutatua matatizo yoyote yanayojitokeza katika sekta hii ya misitu katika ngazi mbalimbali za uzalishaji wake,” alisema.

Mkurugenzi wa FDT Simon Milledge alisema katika kusaidia kuboresha sekta ya misitu nchini, taasisi hiyo imejidhatiti katika kuwapatia elimu ya upandaji na utunzaji wa misitu; wakulima wa Nyanda za Juu.

Alisema shambo lao la mafunzo la Kisolanza linatoa ushahidi tosha kwamba matumizi ya mbegu bora zilizofanyiwa utafiti zinazoweza kutoa mazao bora na kwa wingi kwa kuzingatia hali ya hewa na udongo wa maeneo husika.


Alisema FDT inataka kuona sektta ya misitu inakuwa kimbilio la wakulima wengi wakiwemo wanaotoka katika kaya masikini kutokana na ukubwa wa mapato yake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment