Sunday, 31 January 2016

MAI KUFANYA UTAFITI WA KERO ZA BIASHARA KATIKA MIKOA YA SAGCOTWADAU wa sekta ya biashara katika mikoa mitano iliyopo katika Ukanda wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kwa kushirikiana na taasisi zingine nyeti nchini wameanzisha mtandao utakao tafiti kero za kibiashara katika mikoa hiyo na kuziwakilisha serikalini ili zifanyiwe kazi.

Mwenyekiti wa mtandao huo ujulikanao kama Multi Actors Integration (MAI), Lucas Mwakabungu aliwataja wadau hao kuwa ni pamoja na Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) ya mikoa ya Iringa, Morogoro, Mbeya, Njombe na Ruvuma ambayo yote ipo katika ukanda huo wa SAGCOT.

Alizitaja taasisi zingine zilizopo katika mtandao huo kuwa ni pamoja na Umoja wa Vyuo Vikuu Nchini, vyombo vya habari na washirika wengine katika sekta ya biashara na kilimo likiwemo Jukwaa la Wadau wa Kilimo Tanzania (ANSAF), taasisi inayojihusisha na kilimo cha mbogamboga, matunda na maua nchini (TAHA) na mpango wa SAGCOT wenyewe.

Alisema kwa kupitia ufadhili wa shirika la BEST AC mpango huo utafiti ambao ni mpango wa majaribio wa mwaka mmoja katika mikoa hiyo, utafanywa pia katika mikoa mingine ili kuoanisha matokeo yake.

Mwakabungu alisema wadau hao watakaokutana mara mbili kwa mwaka wataongozwa na wawakilishi kutoka umoja wa vyuo vikuu kufanya utafiti huo na kutoa ushauri wa kuondoa vikwazo vya biashara serikalini ili iweze kuboresha mazingira mazuri ya biashara.

“Tumekutana hapa Mbeya kwa siku mbili na kuainisha baadhi ya kero zinazoigusa sekta ya biashara. Kero hizo zitapelekwa katika vyuo hivyo vikuu ili zifanyiwe utafiti kabla ya kupelekwa serikalini kwa ajili ya kuzishughulikia,” alisema.

Alizitaja baadhi ya kero hizo ambazo ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya biashara na wafanyabiashara wenyewe kuwa ni pamoja na wingi na ukubwa wa kodi na mikopo yenye riba kubwa.

Mwakabungu alisema utafiti wao wa awali unaonesha katika biashara moja nchini kuna kodi zaidi ya 20 huku wenye viwanda wakirundikiwa kodi zaidi ya 30 kwa mwaka jambo linalopunguza idadi ya walipa kodi badala ya kuongeza wigo wa walipa kodi.

Kwa upande wake, Dk Goodluck Urassa wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Biashara alisema serikali inakila sababu ya kuboresha mazingira ya biashara ili yatanue wigo wa ajira nchini.

Alisema kwa kupitia program ya BEST ambayo inalenga kuboresha mazingira ya biashara nchini watasaidia kuibua mambo mbalimbali yanayoongeza kero kwa wafanyabiashara na kufanya utetezi.

“Tunashughulikia mambo ya kodi za mazao, vipimo, bidhaa feki, pembejeo feki. Tunafanya utafiti, tunatoa mafunzo na tunatoa ushauri na kufanya mazungumzo na serikali ili kuiboresha sekta hii ya biashara,” alisema.

Akitoa mfano wa tafiti zilizofanywa kwa kupitia program ya BEST, Dk Urassa alisema; “mwaka 2012 tulifanya utafiti wa vipimo vya mahindi na mpunga na kubaini serikali na wakulima wenyewe wanapoteza fedha nyingi kwasababu ya ujazo wa ziada maarufu kama lumbesa.”

Alisema utafiti wao kuhusu vipimo vya Lumbesa unaonesha serikali imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh Bilioni 14.8 kama mapato ya kodi huku wakulima nchini kote wakipata hasara ya zaidi ya Sh Bilioni 174 kila mwaka.


Aliutaja utafiti mwingine wanaoendelea nao hivisasa ambao matokeo yake yatatolewa Februari mwaka huu kuwa ni pamoja na matumizi ya pembejeo feki mkoani Njombe na athari ambazo serikali na wakulima wanapata.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment