Wednesday, 13 January 2016

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI ZUIO LA UCHAGUZI WA MEYA NA NAIBU MEYA ILALA NA KINONDONI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Hatimaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali ombi la zuio la muda la kufanyika kwa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya kwa Wilaya za Kinondoni na Ilala baada ya mlalamikaji kushindwa kuwasilisha hati za madai kwa upande wa walamikiwa ndani ya muda muafaka.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi, Respicius Mwijage alisema kuwa mlalamikaji alifungua kesi chini ya hati ya dharura akiiomba mahakama itoe zuio la muda kwa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya lakini inashangaza kuwa alishindwa kuwasilisha hati ya madai kwa walalamikiwa ili kukidhi matakwa ya kisheria na uharaka wa kesi hiyo kama alivyoomba.

“Mlalamikaji alikuwa anajua uharaka wa kesi hii na hajaonyesha sababu yoyote ya msingi iliyomfanya kushindwa kuwasilisha hati ya madai kwa upande wa walalamikiwa hadi leo hii kesi ilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa,” Hakimu aliongeza.

Akisisitiza uamuzi huo wa mahakama, Hakimu Mwijage alisema mashauri ya uchaguzi ni mashauri yanayohusu jamii kwa ujumla na muda ni suala la msingi sana hivyo mahakama haiwezi kuvumilia hali hii na kuamua kutupilia mbali ombi la mlalamikaji kwa kushindwa kuwasilisha hati ya madai kwa walalamikiwa.

Wakati huohuo mlalamikaji katika kesi hiyo Elias Philemon Nawera amewasilisha ombi la kuondoa kesi hiyo ya msingi mahakamani kwasababu ya ukweli kwamba ni jambo linalohusu jamii nzima, na kwamba muda ni suala la msingi kwani kuna idadi kubwa ya watu ambao wanaendelea kuadhirika kwa kutokuwa na Meya na Naibu Meya na kuomba kila upande ugharamie gharama za kesi kwa upande husika.

Naye Hakimu Mwijage akaifuta kesi hiyo baada ya upande wa walalamikiwa kuridhia ombi la mlalamikaji la kuondoa kesi hiyo mahakamani bila ya gharama za fidia.

Mnamo Januari 8, mwaka huu mlalamikaji Elias Philemon Nawera alifungua kesi ya uchaguzi chini ya hati ya dharura dhidi ya Wakurugenzi wa Manispaa za Ilala na Kinondoni akiiomba mahakama kusikiliza kesi kwa upande mmoja na kutoa zuio la muda la kuwazuia walalamikiwa wasiendelee na uchaguzi wa Meya na Naibu Meya uliokuwa umepangwa kufanyika siku iliyokuwa inafuata, Jumamosi ya January 9, mwaka huu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment