Wednesday, 27 January 2016

KESI DHIDI YA MEYA WA KINONDONI YAIVA DAR ES SALAAM

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob

UPANDE wa Jamhuri umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi katika kesi inayomkabili Diwani wa Kata ya Ubungo na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob anayetuhumiwa kumpiga na kumjeruhi Mwandishi wa Habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lissa, umekamilika.

Mshtakiwa anatakiwa kufika mahakamani hapo Februari 4, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, Wakili wa Serikali Keneth Sekwao, amesema alifikishwa mahakamani hapo akidaiwa kutenda kosa la kumpiga mateke sehemu mbalimbali za mwili na kumjeruhi mwandishi huyo katika tukio lililotokea Septemba 15, mwaka jana, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo lililotokea makao makuu ya Chadema, mwandishi huyo alijikuta katika msukosuko huo baada ya kuonekana akiwa na kundi la wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliodaiwa kujifanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana kumpinga Mgombea Urais kupitia Chadema, Edward Lowassa.

Pamoja na kutuhumiwa kumjeruhi mwandishi, mshtakiwa anadaiwa kuharibu kamera aina ya Nikon yenye thamani ya Sh Milioni 8, ambayo pia ni mali ya Uhuru Publications Limited (UPL).

Mshtakiwa amekana mashtaka yote dhidi yake huku akisisitiza nje ya mahakama kwamba ilitengenezwa kulingana na upepo wa kisiasa uliokuwa unaendelea kwa wakati huo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment