Wednesday, 27 January 2016

KAYA MASIKINI KILOLO ZAMWAGIWA MAMILIONI MENGINE YA TASAF
KAYA masikini 6,490 za vijiji 70 vya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa zimepata malipo ya nne ya zaidi ya Sh Milioni 198.5 wiki hii yatakayoziwezesha  kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamua mahitaji yao muhimu.

Fedha hizo zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) zinazifanya kaya hizo ziwe zimepata zaidi ya Sh Milioni 800 tangu mpango huo uanze, Julai mwaka jana.

“Zaidi ya Sh Milioni 800 zimeletwa wilayani Kilolo kwa ajili ya kuzinusuru kaya hizo, ni matarajio yetu fedha hizo zitasaidia kubadili maisha ya watu wa Kilolo kama ilivyokusudiwa,” alisema Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Kilolo, Venance Mwaikambo wakati shughuli ya kugawa fedha hizo ikiendelea jana.

Mwaikambo alisema litakuwa jambo la kushangaza kama baadhi ya kaya zinazonufaika na mpango huo zitaonekana hazijabadilika.

“Serikali haijaleta fedha hizi kama zawadi, inataka mtoke kutoka hatua moja muende hatu hatua nyingine,” alisema huku baadhi ya kaya zikikiri kuanzisha miradi midogo midogo ya ufugaji na kilimo kwa kutumia fedha hizo.

Alisema ni makosa fedha hizo kutumika kwa starehe au michango mbalimbali inayohimizwa katika maeneo wanayotoka.

Kwa kupitia mpango huo, Mwikambo alisema kaya hizo zina fursa ya kuboresha maisha yao kwa kutumia akiba ya fedha wanayoweza kuipata kutoka katika Sh 20,000 na zaidi ya Sh 70,000 wanazopata kila baada ya miezi miwili.

Afisa ushauri na ufuatiliaji wa mpango huo wa TASAF wilayani Kilolo, Happy Mpuya alisema serikali kwa kupitia mpango huo inatoa ruzuku ya msingi na ya masharti nafuu kwa kaya masikini ili kugharamia mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya na maji.

Mpuya alisema ruzuku ya msingi inatolewa kwa kila kaya iliyoandiskishwa kwenye mpango ili kugharamia mahitaji hayo ya msingi na ruzuku ya masharti nafuu inatolewa kwa kaya masikini zenye watoto wenye umri wa kwenda shule na kliniki.

“Mpango unalenga pia kutoa ajira ya muda kwa kaya hizo na zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi wakati wa kipindi cha hari na majanga mbalimbali kama vile ukame na mafuriko,” alisema.

Alisema kaya zitakazobainika kuzitumia fedha hizo kinyume na malengo hayo zitaondolewa katika mpango kama masharti ya mpango yanavyotaka fedha hizo zisitumike kwa shughuli nyingine tofauti na za mpango.

Mmoja wa walengwa wa mpango huo, Lickson Chambaga (70) wa kijiji cha Luganga aliyepata jumla ya Sh 80,000 toka Julai mwaka jana alisema; “kwa kupitia akiba ya Sh 30,000 niliyojiwekea, nilinunua kuku tetea wawili na jogoo mmoja. Hivi sasa nina kuku 14 ambao watanipa faida kama nitawauza baada ya kukua vizuri,” alisema.

Alisema kuku hao anawafuga kienyeji kwahiyo hana gharama yoyote ya ziada ya kuwatunza kama hawatashambuliwa na magonjwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment