Saturday, 9 January 2016

KAULU YA SERIKALI KUHUSU NYUMBA YA MAMA LWAKATARE


Mkutano ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji Rwakatare.  Ilielezwa kwamba Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume kabisa na Sheria tatu muhimu. 

 Pia ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. 

Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani. Wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11 Mei 2015, aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza, kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.  

 Makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei 2015. Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo.

 Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa zake zimekwishafikishwa TAKUKURU. 

Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais, iliiagiza Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba “makubaliano” kati yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na njia ya udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe 29 Disemba 2015.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment