Sunday, 17 January 2016

JESHI LA POLISI IRINGA LAWANASA WAHAMIAJI HARAMU 83, WALIKUWA WAKITOKEA KONGOWE DARJESHI la Polisi Mkoani Iringa limewatia mbaroni wahamiaji haramu 83, raia wa Ethiopia, waliokuwa wakisafirishwa na roli Scania T478 DFE mali ya Frola Mwambenja kutokea Kongowe Dar es Salaam wakielekea Kyela mkoani Mbeya.

Pamoja na wahamiaji hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Peter Kakamba aliwaambia wanahabari jana kwamba jeshi hilo linamshikilia pia dereva wa roli hilo, Hans Mwakyoma (28) mkazi wa Tukuyu Mbeya na msaidizi wake Alex Adam (32) mkazi wa Mbeya mjini, kwa tuhuma za usafirishaji wa watu hao.

Kamanda Kakamba alisema gari hilo lilikamatwa na askari wa doria wa jeshi hilo majira ya saa 3.30 usiku katika kijiji cha Mahenge kitongoji cha Kibotora, barabara kuu ya Iringa Mbeya likiwasafirisha watu hao kuelekea Kyela ambako ni mpakani mwa Tanzania na Malawi.

“Lilipokamatwa roli hilo, dereva alisema halina mzigo, lakini askari wetu walipolifungua walikuta watu hao wakiwa wamelaliana, baadhi yao wakiwa na hali mbaya na wengine wakiwa wagonjwa,” alisema.

Alisema baada ya kuwakamata, wahamiaji hao walipewa chakula na wale walioonekana wagonjwa wamepatiwa matibabu wakati taratibu zingine za kuwafikisha katika vyombo vya sheria zikiendelea.

“Jambo la kushangaza ni kwamba watu hao walipakiwa katika gari hilo Kongowe jijini Dar es Salaam. Kila mtu anajua Kongowe sio Ethiopia kwahiyo kuna swali la kujiuliza ni namna walivyofika Kongowe hadi wakapata huduma ya kusafirishwa kuelekea wanakoelekea,” alisema.

Alisema biashara haramu ya usafirishaji watu  ni jipu kubwa linalohitaji nguvu ya pamoja katika kutumbuliwa kwani inahusisha mtandao wa watu wengi ndani na nje ya nchi.

Alisema katika kupambana na biashara hiyo, taarifa fiche za kiintelejensia za jeshi hilo zinaelekea kuunasa mtandao wa biashara hiyo na lengo hilo litakapofanikiwa wahusika wake watatumbuliwa majipu hadharani.

Alisema watu hao wamekuwa wakiitia gharama kubwa serikali kwani bada ya kuwakamata imekuwa ikilazimika kuwahudumia na kuwasafirisha hadi watokako.

Kamanda Kakamba amewaagiza askari wa jeshi hilo mkoani hapa kuwa makini zaidi katika kulishughulikia suala hilo na mengine ya kihalifu kwani hataki mkoa wake uwe mmoja katika mikoa inayopitisha watu hao.

“Leo mnawaoana watu hawa kama ni watu wanaohangaikia maisha yao, lakini hamuwezi kujua ya moyoni mwao katika kipindi ambacho dunia nzima inapambana na masuala mbalimbali ya kiuhalifu vikiwemo vitendo vya kigaidi,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment