Monday, 4 January 2016

DHI NUREYN ISLAMIC FOUNDATION YATUMIA MILIONI 73 KUSAIDIA FAMILIA 45 ZINAZOJISHUGHULISHA MJINI IRINGA

TAASISI ya Kiislamu ya Dhi Nureyn Islamic Foundation ya mjini Iringa kwa kupitia ufadhili wa taasisi ya RAF ya nchini Qatar imetumia zaidi ya Sh Milioni 73 kutoa mitaji, vifaa na vitendea kazi kwa familia 45 zenye uhitaji mjini hapa.

Sifa kuu iliyoziwezesha familia hizo kupata msaada huo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo, Shamsi Elmi ni kwamba ni za maisha ya chini na zinazofanya shughuli ndogondogo za kibiashara huku zikiwa hazina sifa ya kuishi kama ombaomba.

Msada huo unaohusisha fedha taslimu ambazo ni kati ya Sh 400,000 na sh Milioni 3 kwa familia hizo zenye jumla ya watu 200 umewawezesha pia baadhi yao kupata vifaa na vitendea kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na majokofu, cherehani, vifaa vya kuchomelea na uselemala, vifaa vya mahotelini na pikipiki.

Kazi ya kukabidhi msaada huo kwa walengwa hao ilifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera nje ya msikiti wa Wilolesi wa mjini Iringa, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi hiyo.

Akikabidhi msaada huo Kasesera alisema; “ili mtu awe mwema ni lazima ajali watu wengine, awe mwema kwa yatima, ajali watumishi na masikini, apende watoto, vijana na wazee, mtu huyu aheshimu wazazi wake na wasio wake.”

Aliipongeza taassisi hiyo na wafadhili wake kwa msaada huo akisema wanatekeleza kwa vitendo maagizo na yale yote ya kupenda watu yaliyokuwa yakifanywa na Mtume Mohamed wakati wa uhai wake.


Kasesera aliwataka wanufaika wa msaada huo wautumie kwa malengo yaliyokusudiwa ili waweze kuboresha shughuli zao za maendeleo na maisha yao kwa ujumla.

“Kwa vile msaada huo mmepewa kama familia, jadilianeni kwa pamoja namna ya kuboresha biashara zenu ili msitumbukie kwenye hasara,”alisema.

Awali Katibu Mkuu wa Dhi Nureyn Islamic Foundation alisema kwa kupitia mpango huo unaolenga kuwanufaisha watu wengi zaidi, taasisi yao imepanga kuziwezesha familia mbalimbali katika maeneo mbalimbali wanayofanya kazi kupata fursa ya kupanua biashara zao na kujikwamua kutoka katika kipato duni.

“Ili lengo hilo lifikiwe, taasisi itakuwa inawafuatilia wanufaika wote na kuwasaidia zaidi ili waondokane na utegemezi na hatimaye waishi maisha bora kwa kutegemea kipato wanachopata,” alisema.

Shamsi alisema msaada huo una sharti moja tu kubwa la kuhakikisha vifaa, vitendea kazi au fedha taslimu wanazopewa zinatumika kwa matumizi ya mradi husika ulioombewa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment