Sunday, 17 January 2016

DAILY BREAD LIFE TANZANIA YATIMIZA MIAKA 10, YAPANGA KUANZISHA CHUO KIKUU IKIJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

BAADA ya kuanzisha huduma ya elimu ya sekondari na vituo vya kulea watoto yatima mkoani Iringa, shirika la Daily Bread Life Tanzania (DBLT) limedhimisha miaka 10 ya huduma zake huku likiahidi kuanzisha chuo kikuu na vyuo vya ufundi vitakavyotoa mchango wa kimaendeleo kwa Taifa.

Maadhimisho hayo yaliyowashirikisha wahisani wake toka Marekani yalifanyika juzi katika kituo chake cha watoto yatima cha Daily Bread Life Childrens Home cha mjini Iringa.

Mbali na kito hicho, DBLT inendesha pia kituo kingine cha watoto yatima cha Daily Bread Asante Sana Nzihi kilichopo katika kijiji cha Nzihi, Iringa Vijijini na shule ya sekondari ya Bread of Life iliyopo kijiji cha Mgera Kiwele, Iringa Vijijini.

Mkurugenzi Mkuu wa DBLT, Mchungaji Mpeli Mwaisumbe alisema tangu mwaka 2005 shirika hilo la kidini, limekuwa likijishughulisha zaidi na tafiti zilizoliwezesha kuja na malengo ya kuanzisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo na utoaji wa misaada ya moja kwa moja kulingana na mahitaji na uwezo wa taasisi.

Mchungaji Mwaisumbe alisema baada ya kufanikiwa kuanzisha vituo vya kulea watoto yatima na shule hiyo ya sekondari, malengo yao kwasasa yameelekezwa katika ujenzi wa vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.

“Lengo letu ni kutoa mchango wa moja kwa moja kupitia program za maendeleo za kujikomboa kiuchumi  hasa kwa jamii ya watu waishio vijijini,” alisema.

Alisema wakati kituo cha kulea watoto yatima cha mjini Iringa kina watoto 40,  kile cha Nzihi kina watoto 16 wanaosoma shule za msingi na sekondari zilizopo maeneo yanayozunguka vituo hivyo.

Mmoja wa wahisani wa shirika hilo, Kip Miller ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Eastern Industrial Supplies ya Marekani alisema; “watoto yatima wanatakiwa kulindwa, wanatakiwa kutumikiwa na wakitumikiwa vizuri ipo siku nao watawatumikia watanzania.”

Miller alisema katika maisha yake amefurahi kuona moja ya taasisi (DBLT) inayopata ufadhili kutoka kwao inatumia kile inachopata kwa maendeleo na faida ya watoto wa kitanzani na familia zao.

Alisema watanzania wanatakiwa kuwa waaminifu kama Mungu anavyotaka ili waweze kufikia mafanikio wanayoyataka katika maendeleo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera alilipongeza shirika hilo akisema; “ni watu wachache sana nchini wanapokea fedha za wahisani na kuzitumia kwa usahihi kutekeleza malengo yake.”

Kwa kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Martin Muluwafu alisema serikali itahakikisha shirika hilo linakuwa katika mazingira mazuri  wakati likitekeleza majukumu yake.


Mengine yanayotekelezwa na DBLT ni pamoja na kuchangia shughuli za ufugaji na kilimo katika familia masikini, utoaji wa elimu ya Ukimwi na ujasiriamali na ushauri wa shughuli za kiuchumi na umuhimu wa jamii kubadili tabia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment