Tuesday, 5 January 2016

CWT YAPELEKA UJUMBE MZITO KWA DK MAGUFULI, YATAKA NYONGEZA YA MISHAHARA KWA ASILIMIA 100CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeiomba serikali ya Dk John Magufuli kupandisha mishahara ya walimu kwa asilimia 100 katika kipindi hiki ambacho wanahofia baadhi ya walimu nchini kufukuzwa kazi endapo watatumia vibaya sehemu ya Sh Bilioni 137 zilizotolewa kugharamia utoaji wa elimu ya bure.

Ombi hili lilitolewa na Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Iringa, Stanslaus Mhongole alipokuwa akizungumza na wanahabari katika salamu zake za kuukaribisha mwaka mpya ambazo pia zilitolewa na viongozi mbalimbali wa chama hicho mkoani hapa.

“Hatutaki kuwapoteza walimu wetu popote pale. Ombi langu tuache tabia ya ununuzi wa vifaa hewa pindi tutakapopokea fedha hizo kwasababu tabia hiyo ipo; tukiendelea na tabia hiyo katika serikali hii na kwa kupitia utaratibu huu mpya wa utoaji wa elimu, hakika tutapoteza kazi,” alisema.

Taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Lindi hivikaribuni inaonesha serikali imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu bure toka chekechea hadi kidato cha nne katika kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu.

Wakati zikiwa zimeanza kusambazwa mashuleni ili shule zitakapofunguliwa wanafunzi waanze kunufaika na mpango huo ulioahidiwa na Rais Dk Magufuli wakati wa kampeni zake za urais mwaka jana, taarifa hiyo inaonesha serikali imetoa maelekezo kwa wakurugenzi wa halmashauri pamoja na maafisa elimu na kuwaonya kuhusu matumizi ya fedha hizo.

Mhongole alisema ili walimu hao wanusurike na matumizi mabaya ya fedha hizo kuna umuhimu kwa serikali hiyo kuongeza mshahara wa walimu kwa asilimia 100; ombi ambalo pia lilitolewa wakati wa utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete pamoja na kwamba halikufanyiwa kazi.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya CWT Taifa kutoka mkoa wa Iringa, Pius Kiwele alisema kwa kuanzia wanataka kima cha chini cha mashahara wa walimu kiwe Sh 600,000 kwa mwezi.

Wakati Kiwele akipendekeza kima cha chini kwa walimu kiwe kiasi hicho, kumekuwepo na taarifa kutoka kwa baadhi ya walimu waliopokea kwa masikitiko makubwa tangazo la rais la kufuta kwa michango mbalimbali mashuleni; kwani michango hiyo kwa kiasi fulani ilikuwa ikiwaongezea morali ya kazi kwa kuwa walikuwa wananufaika nayo.

“Bahati waliyona walimu ni kwamba serikali hii ni ya walimu; Rais Dk Magufuli ni mwalimu na mkewe ni mwalimu pia, Waziri Mkuu ni mwalimu na mkewe naye ni mwalimu, kwahiyo ni imani yetu watayapa kipaumbele matatizo yetu,” alisema Mhongole.

Alisema ndoto ya serikali ya kuhakikisha kiwango cha elimu nchini kinafikia ubora unaotakiwa itatokea iwapo serikali itayamaliza manung’uniko ya muda mrefu ya walimu nchini na kubwa kuliko yote ni maslai duni wanayopata wengi wao.

Alisema kama walimu wengi wataendelea kuishi kwa viwango vya mshahara wa sasa ni dhahiri kwamba wengi wao watashindwa kumudu kugharamia mahitaji yao mbalimbali ya msingi kabla hawajapata mshahara mwingine.

“Serikali bado haijafanyia kazi kwa kiwango kinachotakiwa mahitaji mbalimbali ya walimu, morali wa kazi unashuka, inaendelea kutengeneza madeni mbalimbali na inachelewa kuyafanyia kazi maelekezo ya nyaraka mbalimbali za elimu,” aliongeza Kaimu Katibu wa CWT Mkoa wa Iringa, Samwel Mhaiki.

Mbali na kupandisha mishahara yao, Mhongole alisema walimu wanataka madai yao mbalimbali yakiwemo madeni ya malimbikizo ya mishahara, likizo na uhamisho, posho za kufundishia, posho za madaraka na kuchelewa kupandishwa madaraja; yashughulikiwe.


Naye mjumbe wa kamati ya CWT mkoa wa Iringa anayewakilisha walimu walemavu, John Ndumbaro alisema mkoa wa Iringa una walimu walemavu 117 wanaokutana na changamoto mbalimbali kazini ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundombinu rafiki na wao sehemu za kazi, ukosefu wa vifaa vya kujimudu, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment