Wednesday, 13 January 2016

BILIONI 459 ZAWANUFAISHA WANAFUNZI 122,486 ELIMU YA JUU 2015/2016


BODI ya Mikopo Tanzania itatumia zaidi ya Sh Bilioni 459 kutoa mikopo kwa wanafunzi 122,486 wa vyuo vikuu mbalimbali katika msimu wa masomo wa 2015/2016 .
Mikopo hiyo inaelezwa kuvunja rekodi ya mikopo yote iliyowahi kutolewa na chombo hicho tangu kianze kazi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na bodi hiyo leo imesema wanufaika wakubwa wa mikopo hiyo ni wale wanaosoma programu za kipaumbele ambazo zimetajwa katika mwongozo uliotolewa na bodi hiyo mwezi Mei, 2015.

Programu hizo ni Udaktari wa binadamu, udaktari wa wanyama, ufamasia na uuguzi na ualimu wa masomo ya sayansi na hesabu na uhandisi wa umwagiliaji. Wanufaika wengine ni yatima na walemavu.

Katika mwaka uliopita wa masomo, 2014/2015, Serikali kupitia Bodi ilitoa jumla ya Tshs 341/- bilioni zilizowanufaisha wanafunzi 99,069.

Kati ya fedha zilizotolewa, jumla ya Tshs 199.7 bilioni zinakwenda kwa wanafunzi 53,537 waliojiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza mwezi Novemba, 2015  katika vyuo mbalimbali na Tshs Tshs 259.1 bilioni zinalipwa kwa wanafunzi 68,916 wanaoendelea na masomo, yaani mwaka wa pili, wa tatu na kuendelea katika vyuo vya umma na binafsi.

Katika hatua nyingine, Bodi ya Mikopo inatoa wito kwa waajiri katika taasisi za umma na binafsi nchini kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria iliyoanzisha Bodi inayowataka kuwatambua waajiriwa wao ambao ni wanufaika wa mikopo inayotolewa na Bodi; kukata sehemu ya mishahara yao na kuwasilisha kwa bodi kama marejesho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Bodi, Kifungu cha 20 (1) (c) cha sheria ya iliyoanzisha Bodi (Higher Education Students’ Loans Board Act (as amended)), kinawataka waajiri kuwatambua waajiriwa, kuijulisha Bodi kwa maandishi ndani siku 28 tangu wapate ajira. Aidha, Kifungu cha 20 (2) cha sheria hiyo, kinawataka waajiri, baada ya Bodi kuthibitisha kuwa muajiriwa ni mnufaika wa mikopo ya Bodi, (mwajiri) kuitaarifu kuitaarifu Bodi, ndani ya siku 30 za ajira yake na kukata makato kutoka katika mshahara wa mwajiriwa na kuyawasilisha Bodi ndani ya siku 15 baada ya kila mwisho wa mwezi.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa waajiri wote wanapaswa kutimiza matakwa hayo ya kisheria na kuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza kukagua taaasisi za umma kama zinazingatia matakwa haya ya kisheria.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005. Bodi ina majukumu kadhaa, lakini mawili makubwa ni kutoa
mikopo kwa wanafunzi watanzania wahitaji; na kusimamia urejeshaji wa mikopo
kutoka kwa wanufaika wa mikopo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment