Wednesday, 9 December 2015

WAMUOMBA DK MAGUFULI KUUNDA SERIKALI NDOGO WAKATI WAKIING'ARISHA OFISI YA CCM MKOA WA IRINGA

VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa wamesema wanaunga mkono azma ya Rais Dk John Magufuli ya kuunda baraza dogo la mawaziri litakalokuwa na ufanisi na tija kwa maendeleo ya watanzania.

Wakiungana na watanzania nchini kote kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru kwa kufanya usafi katika maeneo yao na yale ya kutolea huduma, viongozi hao walisema kama lingekuwa si suala la kikatiba, kwa kazi na kasi ya utendaji  iliyooneshwa na serikali ya Dk Magafuli, hawaoni haja ya kuwa na baraza la mawaziri na kwamba kazi zao zinaweza kufanywa na makatibu wakuu.

“Tunaona Rais, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue wanavyoitekeleza Ilani ya CCM bila uwepo wa mawaziri.Kila mahali viongozi hao wanapata pongezi, kazi wanayofanya ni kubwa mpaka wengine wanauliza kama kazi kubwa inaweza kufanywa na wachache kunasababu gani ya kuwa na baraza la mawaziri,” alisema Katibu wa UWT Mkoa wa Iringa, Mwajemi Baragama.

Baragama na Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa wa Iringa, Agnes Ulaya na Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa Alli Nyawenga waliwaongoza wanachama na wapangaji wa jengo la ofisi ya CCM Mkoa wa Iringa, mjini Iringa kuling’arisha jengo hilo kwa usafi.

Akielezea jinsi shughuli hiyo ilivyofanikiwa Ulaya alisema; “viongozi wa chama pamoja na wale wa jumuiya zake zote, na baadhi ya wapangaji na wanachama wetu, tulikutana hapa saa 12.30 na kuendelea na usafi hadi saa sita mchana.”

Alisema ndani ya muda huo wamefanya usafi wa mazingira yote yanayozunguka jengo hilo la ghorofa moja na wamekubaliana kazi hiyo maalumu itakuwa ikifanyika kila mwisho wa mwezi pamoja na kufanywa kwa utaratibu wa kawaida kila siku.

Alisema huko nyuma kumewahi kuwepo na maagizo ya kufanya usafi kwa stahili hiyo lakini hakukuwa na mwamko mkubwa kama ilivyojitokeza kupitia agizo la Rais Dk Magufuli.

“Hii ni kwasababu watu wengi wanafurahishwa na utendaji wake na wanapenda kufanya kazi kwa staili anayotaka ambayo kimsingi inalenga kuongeza mwamko wa bidii ya kazi kwa watanzania wote,” Ulaya alisema.

Naye Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa Nyawenga, alitumia maadhimisho hayo kuwataka vijana kuacha utamaduni wa kupiga soga na kufanya mambo yasio na tija wakati wa muda wa kazi.

“Rais wetu anataka watanzania wafanye kazi ili waharakishe maendeleo yao na ya taifa, na tuna imani kwa kasi yake hata zile fedha zinazotakiwa kutolewa na kila halmashauri kwa ajili ya kuwakopesha vijana na wanawake zitaanza kutoka ili wahusika wazitumie kufanya maendeleo yao,” Nyawenga alisema.

Wakati viongozi hao wa mkoa wakisafisha jengo la ofisi zao, waliokuwa wagombea udiwani kupitia chama hicho katika kata zote 18 za Manispaa ya Iringa, wakiwemo wanne walioshinda katika uchaguzi huo, walijitokeza katika kata zao na kushirikiana na wananchi wengine kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment