Tuesday, 8 December 2015

WALIOGOMBEA UDIWANI MANISPAA YA IRINGA KWA TIKETI YA CCM KUHAMASISHA USAFI WA MAZINGIRA SIKU YA UHURUCHAMA cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kimewaita madiwani wake wanne wa kuchaguliwa na wale 14 walioangushwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu kuitikia wito wa Rais Dk John Magufuli wa kusheherekea miaka 54 ya Uhuru kwa kufanya usafi.

Akizungumza na wanahabari leo hii, Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa Elisha Mwampashi alisema;  “Waliokuwa wagombea wetu udiwani wa kata zote bila kujali matokeo ya Uchaguzi Mkuu yalikuwaje watashiriki kuhamasisha na kufanya usafi katika maeneo yao.”

Hivi karibuni Rais Magufuli alifuta sherehe za uhuru za mwaka huu, akisema ni aibu kwa taifa kuadhimisha miaka 54 ya uhuru mwaka huu huku taifa likikabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na uchafu, na ameagiza watendaji wote wa halmashauri na manispaa nchini kuhakikisha wanatayarisha vifaa vya kufanyia usafi ili kila mwananchi aweze kushiriki.

Mwampashi alisema; “CCM Manispaa ya Iringa inaitikia kwa mikono miwili agizo la Rais na katika kusheherekea sikukuu hiyo hapo kesho tunawataka wana CCM wote waungane na watanzania wengine kusafisha maeneo yao,”

Mwampashi alisema pamoja na kusheherekea siku hiyo ya uhuru kwa kufanya usafi, aliitaka halmashauri ya manispaa ya Iringa inayoundwa kwa wingi na madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutunga sheria itakayowahamasisha wana Iringa kutunza mazingira.

“Wenzetu katika mikoa mingine kama Moshi wana utaratibu wa kuwatoza faini watu wanaotupa taka ovyo katika maeneo yasioruhusiwa. Muda umefika na wana Iringa tuwe na sheria hiyo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment