Sunday, 27 December 2015

VIJANA TISA WAANZISHA KAMPUNI, WACHANGISHANA MILIONI 500 NA KUANZISHA KIWANDA CHA KUTIBU NGUZO ZA UMEME

VIJANA tisa wenye vipato vya kawaida kutoka maeneo mbalimbali nchini, wametimiza ndoto ya umoja ni nguvu kwa kuanzisha kampuni ya kizalendo wanayotaka iongoze nchini kwa uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na misitu zitakazo zingatia ubora wa kimataifa.

Vijana hao German Ibreck, Anael Samuel, Prosper Moshi, Edward Masuzya, Edwin John, Baraka Maduhu, Leevan Maro, Beatrice Masalu na Elisha Msengi  wameanzisha kampuni ijulikanayo kama Agora Wood Products Ltd.

Kampuni hiyo iko katika hatua za awali za ujenzi wa kiwanda cha kutibu nguzo za umeme na bidhaa zingine zifananazo na hizo katika kijiji cha Igwachanya, kata ya Mseke, wilayani Iringa.

Jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho kitakachokuwa na uwezo wa kutibu wastani wa nguzo za umeme 200 kwa siku, liliwekwa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hafla iliyohudhuriwa na wananchi wa kijiji hicho, na viongozi wa serikali ya mkoa na wilaya ya Iringa.

Afisa Mtendaji wa kampuni hiyo, Elisha Msengi alisema kiwanda hicho kitatumia teknolojia mpya katika kuwezesha dawa kupenya vizuri ndani ya nguzo na bidhaa zingine zitokanazo na miti na hivyo kuongeza ubora na matumizi ya muda mrefu ya bidhaa hizo.

“Kitakapokamilika, kiwanda kitatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 50 na nyingine 200 zisizo za moja kwa moja,” alisema na kuongeza kwamba kiwanda hicho kitachangia kwa kiwango kikubwa mapato ya fedha za halmashauri na serikali kuu kwa njia ya kodi na tozo muhimu.

Alisema ujenzi wa majengo na miundombinu iliyopo katika kiwanda hicho ulianza Septemba, 2015 ukihusisha ununuzi wa mitambo, ardhi, malighafi za ujenzi na kazi kwa zaidi ya Sh Milioni 500 ambazo zimechangwa na vijana hao.

Alisema hadi kukamilika kwake, kiwanda hicho kitagharimu zaidi ya Sh Bilioni 2.5 na akashangaa mradi huo wenye manufaa makubwa kwa mkoa na Taifa ulivyokosa mkopo kutoka katika moja ya benki za hapa nchini pamoja na kusubiri kwa miezi tisa tangu mkopo huo uombwe.

Akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema; “natiwa moyo na kufurahishwa sana kuona kwamba kiwanda hiki kimejengwa na kumilikiwa na wazawa kwa asilimia 100.”

Masenza alisema serikali ya awamu ya tano  ya Dk John Magufuli imelenga kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ili badala ya kuuza malighafi, ziuzwe bidhaa ambazo zimetengenezwa kwa ubora na zenye thamani katika soko la ndani na nje.

Alisema ili kufikia lengo hilo serikali hiyo imedhamiria kuondoa ukiritimba ambao umekuwa ukikatisha tamaa wawekezaji wa ndani na nje wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya viwanda.

Ili kianze kufanya kazi kiwanda hicho ambacho mitambo yake ya kutibu bidhaa hizo za miti inaendelea kufungwa, kinahitaji kuunganishwa na umeme wa njia tatu na transfoma na ujenzi wa barabara ya mtaa kuelekea kiwandani.


“Tunawakaribisha Tanesco washirikiane nasi kupitia mpango wa Public Private Partnership, kifedha, kiutaalamu na kiushauri katika kuzalisha nguzo bora za umeme,” alisema Afisa Mtendaji wa kampuni hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment