Thursday, 3 December 2015

UZALISHAJI WA MAZIWA UNAOZINGATIA UBORA WA KWANZA WASHIKA KASI NYANDA ZA JUU

MIKOA ya Iringa, Mbeya na Njombe imeanza kupiga hatua katika uzalishaji wa maziwa unaozingatia ubora wa kwanza kuanzia kwa mfugaji hadi katika hatua ya usindikaji.

Hayo yalisemwa juzi mjini Iringa na Mshauri Mwandamizi wa Uzalishaji wa Maziwa wa Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika Mashariki (EADD) kanda ya Iringa, Ndisha Joseph.

Katika mafunzo ya siku nne yaliyohusisha maafisa mifugo wa wilaya za mikoa hiyo na wasindikaji wa maziwa, Joseph alisema kwa kupitia mradi huo wa miaka mitano ulioanza kutekelezwa mwaka 2014, wafugaji wanapata mafunzo ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa.

Alisema mradi huo unaofadhiliwa na taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation utawasaidia wafugaji 35,000 wa ng’ombe wa maziwa katika mikoa hiyo yenye fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji. 

Alisema Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika Mashariki  unaotekelezwa kwa awamu ya pili katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kwa kutumia mfumo wa Kitovu cha Maziwa (Dairy Hub).

Alisema mradi unatekelezwa kwa ubia-kongano kati ya Heifer International (msimamizi mkuu wa Mradi na kuongeza uzalishaji maziwa) kwa kushirikiana na Technoserve (biashara na masoko ya maziwa); ABS (uboreshaji koosafi za ng’ombe wa maziwa); ICRAF (kuboresha lishe na malisho ya mifugo ) na ILRI (utafiti na mafunzo ili kuongeza ufanisi).

Meneja Biashara wa EADD, Daniel Laizer alisema kwa kuwa mradi unalenga kushughulikia mnyololo mzima wa thamani wa maziwa kuanzia uzalishaji hadi sokoni, ni lazima maziwa yanayopelekwa sokoni yawe yale yanayotakiwa katika masoko hayo.

“Kuna changamoto ambazo wafugaji wanapata katika uzalishaji maziwa, changamoto hizo zinawafanya wakose masoko kwasababu wanachozalisha hakina ubora unaohitajika na soko,” alisema.

Alisema wafugaji wanatakiwa kusaidiwa ili wajue ubora wa maziwa unaotakiwa na sababu zinazoharibu ubora huo ili wawe na uwezo wa kujua mchakato mzima wa uzalishaji maziwa hadi yanapofikishwa sokoni.

Kwa kupitia mradi huo, Laizer alisema vitawekwa vitovu vya biashara ya maziwa katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa hiyo ili kuwawezesha wafugaji kuwa jirani na masoko.

Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alisema sekta ya maziwa ina mchango mkubwa katika uendelezaji uchumi wa watu na Taifa kwa ujumla.


Katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa Martin Muluwafu, Ayobu alisema mradi huo ukifanikiwa wafugaji wengine nchini kote wataiga mazuri yake na hivyo kuiboresha sekta hiyo kitaifa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment