Friday, 18 December 2015

UN TANZANIA YAZINDUA RIPOTI YA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU 2015

IMG_8928

IMG_8949

IMG_8888

Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Alvaro Rodriguez amezitaka serikali za nchi za Afrika ikiwemo serikali ya Tanzania kutekeleza vyema sera ya sayansi, teknolojia na ubunifu na kuhuisha sera ya viwanda kwa ajili ya mipango ya ukuzaji wa viwanda.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwaka 2015 inayohusu Teknolojia na Ubunifu, ambayo imetolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la linaloshughulikia Biashara na Maendeleo (UNCTAD). Shughuli iliyofanyika Chuo cha Diplomasia cha Msumbiji na Tanzania, kilichopo Kurasini Dar es salaam.

Katika hotuba yake hiyo alisema suala la Sera za ubunifu ni mpya kwa mataifa mengi ya Kiafrika na hivyo hazitekelezwi vyema na kusema pia mifumo ya uvumbuzi inakabiliwa na changamoto nyingi.

Alisema sera nyingi za viwanda katika nchi za Afrika hazikujenga mfumo wenye kuchagia mafunzo ya teknolojia na utekelezaji wake.

“Na hata kama kuna sera za maendeleo ya viwanda sera hiyo haikuratibiwa vizuri na suala la sayansi teknolojia na uvumbuzi.” Alisema.

Alisema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuhakikisha kwamba zinaoanisha yote hayo ilikuwa na sera madhubuti ya mazingira yenye lengo la kuendeleza viwanda, teknolojia na sayansi vikiwa pamoja.

Hafla hiyo imefanyika ikiwa ni siku moja tangu Umoja wa Mataifa (UN) kuzindua ripoti inayohusu Teknolojia na Ubunifu duniani 2015 jijini Geneva, Switzerland, ofisi ya UN Tanzania imezindua ripoti hiyo nchini na kuonyesha hali iliyopo Afrika.

Akizungumzia uzinduzi huo, mdadavuzi wa ripoti hiyo, Dkt. Bitrina Diyamett kutokea Taasisi ya Utafiti wa Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STIPRO) alisema katika taarifa hiyo ambayo imeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inaonyesha jinsi ambavyo Tanzania na nchi nyingine za kiafrika zisivyokuwa na sera nzuri za viwanda na ubunifu.

Alisema katika tafiti ambayo imeanza kufanyika mwaka 2000 katika nchi zaidi ya 10 za Afrika kunaonekana serikali za Afrika zinashindwa kutofautisha sera viwanda na sera ya sayansi, teknolojia na ubunifu na hivyo kushindwa kukuza viwanda na kuwasaidia wazalishaji wa nchini sababu sera hizo ndiyo zinazowaunganisha.

Katika utafiti huo uliofanywa na UNCTAD unaonyesha kuwa mauzo ya bidhaa zinazotengenezwa kwa teknolojia ya juu umefikia asilimia 52 mpaka 2014 na umekua kwa asilimia 18 duniani kote kuanzia mwaka 2000 na Afrika umekua kwa asilimia 0.3 kati ya asilimia 18 ambazo zinaonekana kukua tangu 2000.

Aliongeza kuwa ili sera hizo zifanye kazi zinahitaji kushirikiana lakini kwa Afrika hakuna ushirikiano na kuwa katika wakati mgumu ya kuzifanyia kazi sera hizo.
"Wamefanya utafiti lakini Afrika hali sio nzuri shida zilizopo hakuna ushirikiano kila mtu anakuwa kivyake, hawa wanafanya kazi kwa kuangalia sera yao kivyao na hawa wanafanya kivyao kwahiyo kufanikiwa inakuwa shida,

" Ukiangalia kwa Afrika hata katika nchi ambazo zinajitahidi kwa sera hizo kuwa sehemu moja lakini watekelezaji wake hawana umoja kwamba wakae pamoja kuona jinsi wanafanya sasa unakuwa kama ugomvi kila mtu kuona ni sera yake na hakuna kitu kinafanyika," alisema Dkt. Bitrina.

Dkt. Bitrina alisema kutokuwepo kwa ushirikiano kunafanya kupotea kwa fedha nyingi kwa sababu serikali inakuwa inatoa pesa nyingi kutekeleza sera moja na ikitoa tena pesa nyingine kwa utekelezaji wa sera nyingine lakini kama sera hizo zikifanya kazi kwa kushirikiana kuna uwezekano wa kuokoa pesa hizo.

Aidha alitoa ushauri kwa serikali kupitia upya sera ya viwanda na sera ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuzifanya sera hizo kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kuinua viwanda ambavyo ndiyo vinatoa ajira nyingi na kama watafanya hivyo wataweza kupambana na ukosefu wa ajira nchini na kuokoa pesa nyingi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment