Monday, 14 December 2015

RESTLESS DEVELOPMENT YAWAKUTANISHA WANAFUNZI WA VYUO VYA IRINGA NA WAAJIRI


SHIRIKA la kimataifa la Restless Development kwa kupitia program ya Kimataifa ya Huduma kwa Wanafunzi limefanikiwa kwa mara kwanza kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya mjini Iringa katika kongamano ambalo waajiri walizungumzia maarifa wanayotakiwa kuwa nayo wanafunzi hao ili washindane katika soko la ajira.

Katika kongamano hilo lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa, wanafunzi wa chuo cha Ufundi (VETA), chuo cha Biashara Iringa Retco, chuo cha Maendeleo ya Jamii Iringa, na vyuo vikuu vya Mkwawa, Ruaha na Iringa walishiriki.

Mratibu Msaidizi wa shirika hilo, Denice Simeo aliwataja baadhi ya waajiri walioshiriki kuwa ni pamoja na kampuni ya Asas Dairies Ltd, Benki ya Barclays na NMB, kampuni za simu za Tigo na halotel, mashirika ya NSSF na Tuwafikie na wajasiriamali wadogo.

“Kama kuna kipindi kigumu kwa vijana basi ni kipindi hiki ambacho soko la ajira lina ushindani mkubwa kutokana na ufinyu wa nafasi zake unaochangiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza vyuo ambao wengi wao hufundishwa kuajiriwa zaidi kuliko kujiajiri,” alisema.

Alisema tofauti na miaka ya mingi ya nyuma, wanafunzi waliokuwa wakimaliza chuo kikuu walikuwa na uweledi na umahiri mkubwa, hivi sasa nchi ina wanafunzi wengi wanaojiunga na vyuo vikuu ambao waajiri wanasema wengi hawana sifa.

“Katika baadhi ya maeneo sio ajabu kukutana na wahitimu wengi wa vyuo wanaokiri wao wenyewe kutopata maarifa ya kutosha ya kutekeleza ipasavyo majukumu ya kazi iwe katika kuajiriwa au ajira binafsi,” alisema.

Mwakilishi wa kampuni ya Asas Dairies Ltd, Ahamed Kasu alisema pamoja na kwamba katika baadhi ya maeneo imedhihirika kwamba soko la ajira linahitaji watu wenye ufaulu mkubwa badala ya maarifa, yapo mambo ambayo waajiri uyazingatia wakati wakitoa ajira.

Kasu alisema; “mambo hayo ni pamoja na kipaji na uwezo wa kufikiria namna ya kuboresha shughuli za kampuni au taasisi, ubunifu, uwajibikaji na ujasiri.”

Alisema vijana wengi sio wabunifu na hawajiandai kikamilifu wakati wa usaili ili kuwavutia waajiri kwani wengi wao hushindwa kujieleza na hata kutoa historia fupi ya kampuni au taasisi wanayoombea kazi.

Alisema baadhi ya wale wanaofanikiwa kupata kazi, wamedhihirisha katika ajira zao kwamba wao ni watu wa kusukumwa wawapo kazini badala ya kuwa watu wa kujiongoza wenyewe wakati wakitekeleza majukumu yao kila siku.

Naye mjasiriamali Frola Sumaye anayejishughulika na usindikaji wa vyakula vya aina mbalimbali alisema kujiajiri ni jambo linaloimarisha uchumi wa mtu na Taifa kwa ujumla na akawataka vijana wanaomaliza vyuo kujiajiri baada ya kujifunza namna wajasiriamali waliofanikiwa walivyofikia mafanikio waliyonayo.

Kwa upande wa vyuoni, Sumaye alisema inahitajika mikakati mikali ya kuwapa vijana mbinu za kujiajiri kwa kuwapa zaidi mazoezi ya kuwashirikisha kuliko kuwasikiliza tu walimu kama ilivyo hivisasa.

“Yanahitaji mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu kwasababu tumeshindwa kuwawezesha vijana kuishi mitaani na kufanya shughuli za kimaendeleo licha ya kufaulu mitihani,” alisema.

Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa, Faubian George alisema wahitimu wengi wanakosa ujasiri katika soko la ajira kwasababu mambo mengi wanayofundishwa wawapo vyuoni hayawawezeshi kupambana na soko la ajira au kujiajiri.

“Hata katika ujasiriamali, utakuta katika maeneo mengi watu wanatoa mifano na mafunzo ya watu walioajiriwa bila kusema kinagaubaga watu hao walianza vipi hadi kufikia mafanikio waliyonayo,” alisema.

Taarifa ya serikali ya mwaka 2014/2015 inaonesha idadi ya wahitimu wa elimu ya sekondari, vyuo na vyuo vikuu inaongezeka mwaka hadi mwaka huku takwimu za sasa zikikadiria kwamba kati ya vijana 600,000 hadi 800,000 kila mwaka wanaingia kwenye soko la ajira.

Wahitimu hao kwa mujibu wa Restless Development; ni miongoni mwa asilimia 54 ya watu wasio na ajira wenye miaka chini ya 25 katika taifa la 10 duniani kwa kuwa na kundi kubwa la vijana.

Reactions:

1 comments: