Tuesday, 8 December 2015

NEC YATANGAZA TAREHE YA UCHAGUZI WA MAJIMBO YALIYOAHIRISHWA


TUME ya taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza siku ya kupiga kura kwa majimbo ambayo uchaguzi wake ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na Jaji Mstaafu Damian Lubuva inaonesha kura zitapigwa Desemba 13 (Jumapili ijayo) katika majimbo ya Arusha Mjini na Handeni Mjini.

Pamoja na majimbo hayo, kata za Mvomero, Ipala na Nyamwilolewa nazo zitafanya uchaguzi siku hiyo.

Aidha, Jaji Lubuva  amesisitiza kuwa, taratibu zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 mwaka ndizo zitakazotumika kwenye uchaguzi kwenye majimbo hayo na kata hizo.

Ametoa  rai kwa Wananchi wote waliojiandikisha kama wapiga kura katika Majimbo na Kata husika kujitokeza katika vituo walivyojiandikishia ili kuweza kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.

Jaji Lubuva alikumbushia baadhi ya taratibu hizo zikiwemo za mpiga kura kubeba kadi yake ya kupigia kura pindi aendapo kupiga kura, mawakala wa vyama vya siasa lazima wawepo kwenye kila kituo na pia Maafisa Uchaguzi  kufungua kituo na kufunga kwa muda uliopangwa na Tume.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, uchaguzi wa Wabunge na Madiwani wa Majimbo 7 pamoja na Kata 35  ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vifo na vurugu.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment