Sunday, 6 December 2015

MPANGO WA MADIWANI WA CHADEMA IRINGA MJINI WA KUUZA GARI LA MEYA ILI KUNUNUA AMBULANCE WAYEYUKA

Add caption

ULE mpango wa kuuza gari la kisasa lililokuwa likitumiwa na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi ili fedha zitakazopatikana zitumike kununua gari la kubeba wagonjwa kwa ajili ya hospitali ya manispaa hiyo, umeyeyuka.

Gari hilo aina ya Toyota Landa Cruiser Prado New Model linaelezwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh Milioni 150.

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini Iringa kiliwalaumu waliokuwa madiwani wa halmashauri ya manispaa hiyo wa 2010-2015 ambao kwa asilimia 99 walichaguliwa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kupitisha uamuzi waliouita wa kipuuzi wa kununua gari hilo huku hospitali hiyo ikiwa haina gari la kubeba wagonjwa.

Katika mikutano yao mbalimbali ya kampeni Chadema waliwaomba wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini wamchague mgombea wao ubunge na wagombea wake ili wakafanye maamuzi mengi yenye maslai mapana kwa wapiga kura ikiwa ni pamoja na kuuza gari hilo kwa lengo la kutumia fedha zake kununua gari la kubeba wagonjwa.

Ahadi hiyo na nyingine nyingi za chama hicho zilipokelewa na wapiga kura wa mjini Iringa kwa kumchagua kwa awamu nyingine ya miaka mitano Mchungaji Peter Msigwa kuwa mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini na kuwachagua madiwani 14 kati ya 18 wa jimbo hilo, kuunda halmashauri ya manispaa hiyo.

Wakizungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki iliyopita, Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe na Naibu wake Joseph Lyata walisema mpango wa kuuza gari hilo haupo tena kwasababu taratibu za kupata gari la wagonjwa zinaendelea kufanywa kwa kasi kubwa.

“Ni kweli kulikuwa na ahadi ya kuuza gari hili ili fedha zake zitumike kununua gari la wagonjwa, mpango huo haupo tena kwasababu kuna mipango mingine ya kupata fedha zitakazotumika kununua gari rasmi la wagonjwa,” alisema naibu Meya, Lyata.

Lyata alisema kwa kuzingatia mpango huo, gari hilo litaendelea kutumika kwa matumizi ya meya, naibu wake na kwa shughuli zingine za halmashauri pale inapolazimu.

Alisema halmashauri yao itahakikisha inavipitia vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo, zikiwemo kodi mbalimbali, na makusanyo yake yatatumiwa kununua gari la kubeba wagonjwa sambamba na kuongeza gari lingine la kubeba taka ili kuufanya mji wa Iringa uendelee na sifa yake ya usafi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment